Katibu Mtendaji wa taasisi ya Tanzania Cancer Support Hope and Awareness( TCS - HOPE) Bw.Luca Mabena (Kushoto) akiwa pamoja na Mratibu wa Mradi na Mtaalam wa Uelimishaji kuhusu saratani katika taasisi hiyo Emmanuel Chilumba wakizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam.
*******************************
TAASISI ya Tanzania Cancer Support Hope and Awareness( TCS - HOPE) imesema kuna haja ya kuwepo kwa kampeni maalum ya kujenga uelewa dhidi ya mapambano ya saratani nchini ambapo inaelezwa ugonjwa huo unashika nafasi ya nne kwa kusababisha vifo.
Akizungumza leo Septemba 3,2021 mkoani Dar es Salaam Katibu Mtendaji wa taasisi hiyo Luca Mabena amesema kampeni hiyo itaanzaa rasmi Oktoba mwaka huu na wataanza na mikoa ya Kanda ya Ziwa ambako tatizo la saratani limekuwa kubwa.
"Taasisi yetu tumeona haja ya kuwa na kampeni ya kujenga uelewa wa mapambano dhidi ya ugonjwa wa saratani,tunaaamini tukishirikiana kwa pamoja tunaweza kupunguza tatizo la saratani nchini kwetu,kampeni yetu itajikita katika saratani ya matiti na shingo ya kizazi ambayo imekuwa ukiwasumbua wanawake walio wengi,"amesema.
Amefafanua wakati wanaelekea kwenye kampeni hiyo kwa sasa wataanza kwenda kwenye vyombo vya habari kwa ajili ya kuanza kutoa elimu kuhusu saratani kupitia watalaam wa taasisi hiyo ambao watakuwa na mengi ya kueleza kwa umma wa Watanzania.
Mabena amesema kauli mbiu katika kameni hiyo inasema kwamba Uchunguzi wa mapema huokoa maisha huku akisisitiza kupitia kampeni hiyo waanaamini mapambano dhidi ya saratani yatakuwa ya kila Mtanzania."Katika kufanikisha kampeni hii tuko tayari kuchangiwa kupitia namba 336688".
Alipoulizwa kama kuna utafiti wowote umefanyika kufahamu mikoa gani ambayo wakazi wake wana tatizo la saratani ,amejibu utafiti unaonesha mikoa ya kanda ya ziwa tatizo ni kubwa,hivyo hata kampeni yao itaanzia mikoa hiyo.Aidha amesema hakuna sababu ya moja kwa moja inayosababisha saratani.
Akifafanua zaidi kuhusu kampeni hiyo amesema takwimu zinaonesha asilimia 70 wanakuwa wanachelewa matibabu ,hivyo ndani ya kampeni yao watahamasisha wananchi kuwa na uelewa ukiwemo wa kupima afya mara kwa mara na iwapo atabainika kuwa na saratani kuanza matibabu mapema.
Aidha amesema kwamba katika kampeni yao watakuwa wakisambaza jumbe mbalimbali kwenye simu za mkononi pamoja na vyombo vya habari.
Kwa upande wake Mratibu wa Mradi na Mtaalam wa Uelimishaji kuhusu saratani katika taasisi hiyo Emmanuel Chilumba amesema saratani ni maradhi yasiyoambukizwa akitoa mfano wa saratani ya tezi dume na aina nyingine ya saratani.
"Ugonjwa wa saratani nchini unashika nafasi ya nne ukiondoa magonjwa ya moyo, wajawazito ,watoto wachanga pamoja na kushindwa kupumua.Pamoja na mambo mengine tunahamasisha wananchi kupima afya mara kwa mara kwani ukigundua kuwa una saratani mapema ni rahisi kuitibu,"amesema.
Kuhusu taasisi yao amesema inajihusisha na kutoa matumaini na ufahamu na kusaidia masuala yanayohusu ugonjwa huwa na kubwa zaidi wamejikita katika kutoa elimu wakiamini itasaidia kupunguza saratani nchini.
Social Plugin