Muhifadhi wa Makumbusho ya Kihistoria ya Taifa jijini Arusha, Elizabeth Solomoni (kulia) akitoa maelezo kwa wanamuziki waliotembelea makumbusho hiyo.
Na Dotto Mwaibale, Arusha.
SERIKALI imezirejesha tena tuzo kwa wanamuziki wanaotoa kazi bora hapa nchini ili kuwaongezea ari kwenye shughuli zao.
Hayo yalisemwa jana na Afisa Sanaa Mwandamizi kutoka Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Bona Masenge wakati akizindua rasmi Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Muziki Duniani yanayofanyika kwa mara ya kwanza hapa nchini ambayo yalizinduliwa Makumbusho ya Kihistoria ya Taifa jijini Arusha kwa kuandaliwa na Umoja wa Wanamuziki Tanzania (TAMUFO)
Alisema Serikali kupitia Basata wanaandaa tuzo za muziki Tanzania na kuwa tuzo hizo zilikiwa zikitolewa kwa miaka mingi lakini zilisimama na sasa zimeanzishwa tena na ziko kwenye hatua za mwisho.
"Tuzo hizo tutazitoa mapema kabisa na kamati ya kitaifa imekwishaundwa tutazitangaza hivi punde na watu watazisikia," alisema Masenge.
Masenge aliwataka wasanii kuwa wazalendo na kufanya kazi zenye viwango bora kwani lengo la sanaa ni kutoa elimu na burudani na ndio kazi zitakazo wauza kimataifa na kuutambulisha utaifa wetu.
Alisema utamaduni ni roho ya taifa na sanaa yenyewe ni nguzo ya utamaduni hivyo inatakiwa kutambulishwa vema katika ulimwengu na Tanzania kwa ujumla.
Alisema utambulisho huo utakamilika kwa msanii kuwa na nidhamu, kuzingatia muda wa kazi yake,.kutengeneza kazi nzuri itakayo jiuza na si itakayoleta mushikeri katika jamii na kuzingatia maadili kuanzia mavazi na tungo zenyewe.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanamuziki Tanzania (TAMUFO) Stella Joel alisema maadhimisho hayo yaliyofanyika nchi nzima yanakwenda na kauli mbiu ya Muziki ni Kazi Fahari na Urithi wa Utamaduni wetu.
Joel alisema Wanamuziki wa kada zote katika maeneo mbalimbali watashiriki kuhamasisha shughuli mbalimbali za maendeleo kwa mwezi huu wote wa September kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku hiyo Oktoba 1, 2021.
Alisema kwa Arusha walitembelea makumbusho ya Azimio la Arusha na maeneo mengine yenye historia ya nchi.
"Kwa Dar es salaam Wanamuziki walikutana Makumbusho ya Taifa iliyopo Posta ambao wakuwa na jumbe mbalimbali za Kuhamasisha maendeleo ya muziki na kwa Mkoa wa Mwanza walikutana na Kufanya ziara ya Utalii wa Ndani na kujionea vivutio vya utalii wa nchi yetu na kukitangaza Kisiwa cha Sanaane.
Alisema wamechagua Jiji la Arusha kuwa mwenyeji wa uzinduzi wa maadhimisho hayo Kimataifa kwa sababu Mkoa wa Arusha upo katikati ya Afrika pia una Historia kubwa ya nchi yetu ambapo Mhasisi wa Taifa letu Hayati Mwalimu Julius Nyerere alianzisha Azimio la Arusha katika mkoa huo na alitembea kwa miguu na viongozi wengine kuunga azimio hilo na kuwa Arusha ndipo kilipo kiti na mti wa Mwalimu Nyerere.
Joel alitumia nafasi hiyo kuishukuru Serikali, Basata wadau wa muziki, wasanii na makundi mengine kwa ushirikiano mkubwa waliotoa kwa TAMUFO kufanikisha uzinduzi huo.
Alisema katika kipindi hiki cha mwezi huu wasananii mbalimbali jijini Arusha watakuwa wakikutana Hoteli ya Kitalii ya Kibo Palace kwa ajili ya maandalizi na kutoa burudani kuelekea maadhimisho hayo.
Mlezi wa TAMUFO Frank Richard aliwataka wanamuziki kuipeleka Tanzania mbele zaidi kupitia kazi zao kama kauli mbiu ya maadhimisho hayo inavyosema.
Aliwasihi wanamuziki kutunga tungo zenye ujumbe wa kutangaza utamaduni wa nchi yetu na kuzingatia weledi wa kazi zao.
Mwanamuziki Mahiri wa Miondoko ya Zuku Tanzania na mwimbaji wa nyimbo za injili aliyetamba na kibao chake cha presha Hafsa Kazinja alitumia nafasi hiyo kuwaomba wanamuziki wote katika maeneo mbalimbali na wananchi kujitokeza kwa wingi katika kilele cha siku hiyo ya maadhimisho ya kitaifa yatakayofanyika Oktoba 1, 2021.
Kazinja alisema ni muhimu wanamuziki na wananchi kujitokeza kwa wingi katika siku hiyo nadhimu na kuwa wafanye hivyo kama wanavyojitokeza kwenye shughuli zingine kwani siku hiyo ni yao.
Mwanamuziki Mkongwe Komandoo Hamza Kalala alisema katika maadhimisho hayo Arusha itawaka moto hivyo aliwaomba wananchi wajitokeze kwa wingi siku hiyo na ametumia nafasi hiyo kuwaomba wanamuziki kushirikiana na kuzingatia maadili ya kazi zao.
Wakati wa uzinduzi huo Kalala na wanamuziki chipukizi wa jiji la Arusha akiwepo mwanadada anayechipukia kwa kasi katika muziki wa bongo fleva, Dipper Kivuyo kwa jina la kisanii Dipper Rato wa Arusha walikonga nyoyo za waandishi wa habari kwa kuimba vibao vyao kadhaa.
Social Plugin