Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MIGOGORO YA NDOA YATAJWA CHANZO CHA UZURURAJI WA WATOTO,UTORO NA MIMBA ZA UTOTONI MSALALA


Afisa Tathmini na Ufuatiliaji wa Shirika la linalotoa msaada wa kisheria mkoani Shinyanga Paralegal Aid Centre (PACESH), Henerico Masasi akifungua kikao cha Wana Vituo vya Taarifa na Maarifa kata ya Shilela na Lunguya na Wasaidizi wa Kisheria kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Msalala Mkoani Shinyanga kilichoandaliwa na TGNP.

Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Imeelezwa kuwa bado migogoro ya ndoa ni chanzo cha matukio ya ukatili dhidi ya watoto hali inayosababisha watoto kubeba majukumu ya familia na kuchangia utoro wa wanafunzi shuleni, mimba na ndoa za utotoni na uzururaji wa watoto pindi wazazi wao wanapotengana.

Hayo yamebainishwa leo Jumatano Septemba 29,2021 na Wanavituo vya Taarifa na Maarifa Halmashauri ya wilaya Msalala Mkoani Shinyanga wakati wa kikao cha kutoa Matokeo ya Utekelezaji wa Shughuli za Mradi wa Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji wanawake kiuchumi unaotekelezwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwa kupitia shirika la Watu na Makazi Duniani (UNFPA tangu mwezi Julai 2020.

Kikao hicho kilichofanyika katika Ukumbi wa Nitesh Mjini Kahama umehudhuriwa na Wana Vituo vya Taarifa na Maarifa 40 kutoka kata ya Shilela na Lunguya na Wasaidizi wa Kisheria (Paralegals) 25 kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Msalala Mkoani Shinyanga.

Akizungumza katika kikao hicho, Makamu Mwenyekiti wa Kituo cha Taarifa na Maarifa Shilela, Lameck Manyesha amezitaja baadhi ya changamoto wanazoendelea kukabiliana nazo kuwa ni migogoro ya ndoa (kutengana kwa wanandoa) hali inayosababisha watoto kubeba majukumu ya familia na kupelekea utoro wa wanafunzi shuleni, mimba na ndoa za utotoni na uzururaji wa watoto.

“Tunaomba viongozi wa dini wahamasishe wanajamii kufunga ndoa na kuishi vizuri kwani watu waliofunga ndoa wanakuwa na hofu ya Mungu na hawatengani hovyo hovyo kama hawa wanaookotana tu mtaani na kuanza kuishi kama mme na mke matokeo yake wakitengana watoto wanatelekezwa na kuanza kuteseka.

“Pindi wazazi wanapotelezwa wanajikuta wanabeba majukumu ya familia,ikiwemo kulea wadogo zao na wakati mwingine watoto wanajiingiza katika makundi mabaya na wengine kuacha shule na kuanza kufanya biashara ya ngono”,ameeleza Manyesha.

Katibu Msaidizi wa Kituo cha Taarifa na Maarifa Lunguya, Meja John amesema wamefanikiwa kupunguza mila na desturi zisizofaa ikiwemo ya Mila ya Ukango ambapo sasa wachezaji wa ngoma hiyo wameacha kutumia lugha za matusi wanapocheza ngoma zao lakini pia sasa wananchi wameacha kuozesha watoto wa kike katika umri mdogo na sasa pia wanawake wanashiriki kwenye shughuli za uchimbaji madini bila bughudha yoyote.

“Tuliibua choo cha msingi katika shule ya Msingi Lunguya ambacho kilikuwa kibovu. Tukashirikiana na Mwalimu Mkuu na viongozi wa Kijiji na kufanikiwa kujenga matundu 12 ya vyoo (6 kwa ajili ya wasichana na 6 kwa ajili ya wavulana. Pia tumefanikiwa kujengwa kwa choo cha mwalimu Mkuu katika shule hiyo ambapo TGNP imetoa shilingi 600,000 ili kufanikisha ujenzi wa choo hicho”,amesema.

Katika hatua nyingine amesema kata ya Lunguya ina vijiji vitano lakini shule nne za msingi ambazo Madaho, Nyamishiga, Kalole na Kabanda zilizopo hazina walimu wa kike na hakuna vyumba vya kujisitiri kwa watoto wa kike tofauti ya kijiji cha Lunguya.

Naye Msaidizi wa Kisheria Phillip Jackson Sesawanga kutoka kata ya Kashishi Halmashauri ya wilaya ya Msalala amesema Wasaidizi wa Kisheria kwa kushirikiana na Vituo vya Taarifa na Maarifa vinavyosimamiwa na TGNP, wanaendelea kutatua migogoro mbalimbali ya ndoa na ardhi pamoja na kupinga mimba na ndoa za utotoni na kurudisha shuleni watoto wa kike waliokuwa wameachishwa masomo.

Sesawanga ameiomba jamii kuacha kuatamia (kukumbatia) matukio ya ukatili wa kijinsia hivyo watoe taarifa kwa wakati juu ya matukio ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto na hata wanaume wanapofanyiwa ukatili wasisite kutoa taarifa.

Afisa Tathmini na Ufuatiliaji wa Shirika la linalotoa msaada wa kisheria mkoani Shinyanga Paralegal Aid Centre (PACESH), Henerico Masasi amesema kikao hicho kinatoa matokeo na ni kipimo cha kujua ni wapi vituo vya taarifa na maarifa na Wasaidizi wa Kisheria wamefikia katika mapambano ya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto tangu waanze kutekeleza mradi huo mwaka 2020 hadi Septemba 2021.

Amesema kazi kubwa ya Wasaidizi wa Kisheria na Wana Vituo vya Taarifa na Maarifa ni kushughulikia masuala ya ukatili wa kijinsia hasa yanayowakumba zaidi wanawake na watoto ili kuongeza ustawi wa wanawake na watoto katika jamii.

ANGALIA PICHA HAPA CHINI
Afisa Tathmini na Ufuatiliaji wa Shirika la linalotoa msaada wa kisheria mkoani Shinyanga Paralegal Aid Centre (PACESH), Henerico Masasi akifungua kikao cha Wana Vituo vya Taarifa na Maarifa 40 kutoka kata ya Shilela na Lunguya na Wasaidizi wa Kisheria (Paralegals) 25 kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Msalala Mkoani Shinyanga kilichoandaliwa na TGNP leo Jumatano Septemba 29,2021 katika Ukumbi wa Nitesh Mjini Kahama. Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Wana Vituo vya Taarifa na Maarifa 40 kutoka kata ya Shilela na Lunguya na Wasaidizi wa Kisheria (Paralegals) 25 kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Msalala Mkoani Shinyanga  wakiwa kwenye kikao kilichoandaliwa na TGNP
Wana Vituo vya Taarifa na Maarifa 40 kutoka kata ya Shilela na Lunguya na Wasaidizi wa Kisheria (Paralegals) 25 kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Msalala Mkoani Shinyanga  wakiwa kwenye kikao kilichoandaliwa na TGNP.
Makamu Mwenyekiti wa Kituo cha Taarifa na Maarifa Shilela, Lameck Manyesha akiwasilisha taarifa ya kituo hicho ambapo amezitaja baadhi ya changamoto wanazoendelea kukabiliana nazo kuwa ni migogoro ya ndoa hali inayosababisha watoto kubeba majukumu ya familia na kupelekea utoro wa wanafunzi shuleni, mimba na ndoa za utotoni na uzururaji wa watoto.
Katibu Msaidizi wa Kituo cha Taarifa na Maarifa Lunguya, Meja John  akielezea mafanikio waliyoyapata kwenye kituo hicho ikiwamo kupunguza mila na desturi zisizofaa ikiwemo ya Mila ya Ukango ambapo sasa wachezaji wa ngoma hiyo wameacha kutumia lugha za matusi wanapocheza ngoma zao.
Msaidizi wa Kisheria Phillip Jackson Sesawanga kutoka kata ya Kashishi Halmashauri ya wilaya ya Msalala akielezea kuhusu ushirikiano unaofanywa na Wasaidizi wa Kisheria  na Vituo vya Taarifa na Maarifa vinavyosimamiwa na TGNP katika kutatua migogoro mbalimbali ya ndoa na ardhi pamoja na kupinga mimba na ndoa za utotoni na kurudisha shuleni watoto wa kike waliokuwa wameachishwa masomo.
Wana Vituo vya Taarifa na Maarifa  wa kata ya Shilela  wakifanya majadiliano kuhusu Matokeo ya Utekelezaji wa Shughuli za Mradi wa Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji wanawake kiuchumi unaotekelezwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwa kupitia shirika la Watu na Makazi Duniani (UNFPA.
Wasaidizi wa Kisheria kutoka Halmashauri ya wilaya ya Msalala wakifanya majadiliano kuhusu Matokeo ya Utekelezaji wa Shughuli za Mradi wa Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji wanawake kiuchumi unaotekelezwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwa kupitia shirika la Watu na Makazi Duniani (UNFPA.
Wana Vituo vya Taarifa na Maarifa  wa kata ya Lunguya  wakifanya majadiliano kuhusu Matokeo ya Utekelezaji wa Shughuli za Mradi wa Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji wanawake kiuchumi unaotekelezwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwa kupitia shirika la Watu na Makazi Duniani (UNFPA.

Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com