Waziri wa Kilimo Mhe. Prof. Aldolph Mkenda,akizungumza wakati akizindua rasmi Kongamano la Pili la Kimataifa la Ushirika lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU) Septemba 01, 2021 Mkoani Kilimanjaro
Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt. Benson Ndiege akitoa salamu za Ushirika wakati wa uzinduzi Kongamano la Pili la Kimataifa la Ushirika Septemba 01, 2021 Mkoani Kilimanjaro
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ushirika (MoCU) Prof. Alfred Sife akieleza majukumu mbalimbali yanayofanywa na Chuo hicho katika kukuza na kuendeleza taaluma ya Ushirika wakati wa Kongamano la Pili la Kimataifa la Ushirika Septemba 01, 2021 Mkoani Kilimanjaro
Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika Theresia Chitumbi akiongea wakati wa Kongamano la Pili la Kimataifa la Ushirika Septemba 01, 2021 Mkoani Kilimanjaro
Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt. Benson Ndiege (kulia) pamoja na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (Mocu) Prof. Alfred Sife (kushoto) wakionesha mkataba wa ushirikiano baina ya Taasisi hizo (MOU), katikati mwanasheria wa Tume Bw. Shani Mayosa wakati wa Kongamano la Pili la Kimataifa la Ushirika lililozinduliwa Septemba 01, 2021 Mkoani Kilimanjaro.
.............................................................................
Wito umetolewa kwa Vyama vya Ushirika kuangalia namna bora ya kuendeleza viwanda vinavyochakata bidhaa zinazozalishwa na Vyama vya Ushirika kwa kuongeza thamani ya mazao mbalimbali yanayotoka na vyama hivyo ili kuweza kuendana na kasi ya soko la ushindani la ndani na nje ya nchi.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Kilimo Mhe. Prof. Aldolf Mkenda wakati akifungua Kongamano la Pili la Kimataifa la Ushirika katika Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU) mkoani Kilimanjaro. Kongamano hilo limefunguliwa rasmi Jumatano Septemba 01, 2021 hadi Septemba 03,2021 na kuandaliwa kwa ushirikiano wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU) na Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC). Kauli mbiu ya Kongamano ilijikita katika masuala ya Ushirika na Maendeleo ya Viwanda kwa kuzingatia maslahi ya wanachama.
Waziri ameeleza kuwa ni dhamira ya Serikali kuona Vyama vya Ushirika vinaongeza tija kwa kuongeza viwango vya uzalishaji ili iwe ni msukumo wa kuanzisha na kuendeleza Uchumi wa Viwanda kwa kuongeza thamani ya mazao na bidhaa zinazotokana na Vyama, ingawa bado Sekta ya Ushirika inakabiliwa na changamoto zinazopaswa kufanyiwa kazi.
“Lengo la Serikali ni kuimarisha na kuendeleza Ushirika ingawa ushirika unakabiliwa na changamoto za Kisera, masuala ya Sheria, hitaji la wataalamu katika utendaji wa Vyama vya Ushirika,” alisema Prof. Mkenda
Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt. Benson Ndiege katika Kongamano hilo amesema Tume kwa mujibu wa Sheria Na.6 ya mwaka 2013 itaendelea kutekeleza wajibu wa kuvisimamia na kuhamasisha Vyama vya Ushirika
“Ni wakati sasa Vyama vya Ushirika vifikirie kuwa na viwanda vya kuchakata mazao mbalimbali na kuyaongezea thamani ili kuzalisha bidhaa zinazotokana na maziwa, asali, alizeti na mengine mengi,” alieleza Mrajis
Mrajis ameongeza kuwa hivi sasa Sekta ya Ushirika ina viwanda mbalimbali 452 ambavyo vinafanya shughuli mbalimbali za uchakataji. Akibainisha juhudi zinazoendelea katika kuendeleza na kuimarisha viwanda vya Ushirika ni pamoja na uanzishaji wa Kiwanda cha vifungashio katika Chama cha Ushirika SONAMCU mkoani Ruvuma, kiwanda cha ubanguaji Korosho TANECU mkoani Mtwara, Kiwanda ambacho kimeanza kazi ya kuchambua Pamba mkoani Shinyanga kinachomilikiwa na KACU pamoja na vingine.
Akichangia mada wakati wa Kongamano hilo Mtaalamu wa Uchumi Prof. Honest Ngowi ameshauri Vyama vya Ushirika vingi kwa sasa vinazalisha bidhaa na mazao yakiwa ghafi jambo ambalo bado linafanya tija na uchumi wa Vyama kuwa duni.
Aliongeza kuwa uuzaji na usafirishaji wa mazao yaliyoongezwa thamani nje ya nchi unachangia kuongeza pato la Taifa, fursa za ajira, na uchumi wa mtu mmoja mmoja ambao hatimaye utachangia kupunguza umaskini. Akibainisha kuwa hadi kufikia 2020 Viwanda vinachangia ajira kwa kiasi cha asilimia 40. Jambo ambalo likiimarishwa litainua uchumi hasa wa Sekta binafsi na hatimaye Taifa kwa ujumla.
Aidha, Mtaalamu huyo wa uchumi ameeleza kuwa wigo mpana wa vyama vya Ushirika kushiriki katika uchumi na maendeleo ya viwanda kutokana na dhana ya ushirika kuwa yenye uwezo wa kushirikisha Nyanja mbalimbali za uchumi ikiwemo vyama vya ushirika wa kilimo, uvuvi na maeneo mengine.
Pamoja na mambo mengine uzinduzi wa Kongamano hilo ulienda sambamba kwa utiaji saini wa mikataba ya Ushirikiano baina ya Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi na Tume ya Maendeleo ya Ushirika, MoCU na Bodi ya Kahawa, MoCU na Shirikisho la Vyama vya Akiba na Mikopo (SCCULT).
Mada zinazotarajiwa kujadiliwa katika Kongamano hilo ni pamoja na masuala yanayohusu namna bora ya kuonguza uweledi katika utendaji wa vyama, Hifadhi ya Jamii kwa wanaushirika, mabadiliko na maboresho ya Sheria za Ushirika, Ushirikishwaji wa Vijana katika Vyama vya Ushirika zote zikilenga kujadili changamoto ili kupata mapendekezo ya suluhu za kuboresha Sekta ya Ushirika.