MKUTANO WA MWAKA WA NGOs UTAKUWA NI WA KIHISTORIA

 



NA MWANDISHI WETU, DODOMA


MBUNGE wa Viti Maalumu kupitia Asasi za Kiraia Tanzania (NGOs) Neema Lugangira amesema Mkutano wa Mwaka wa Mashirika Yasiyokuwa ya Kiserikali (NGOs) ambao umeandaliwa na Baraza la Taifa la Uratibu wa NGOs kwa maana ya NACONGO kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ambao utakuwa ni wa kihistoria kwa sababu ni kwa mara ya kwanza Rais Tanzania anakutana na Sekta hiyo na Rais huyo ni Mhe Rais Samia Suluhu Hassan.

Aliyasema hayo wakati akizungumza na Waandishi wa Habari ambapo pia  alisema Mkutano huu ni muhimu sana kwa sababu NGOs zinafanya kazi kubwa kwa kushirikiana na Serikali kuchangia kupatikana kwa Maendeleo ya Jamii kwenye maeneo mbalimbali.

Alisema mkutano huo umelenga mambo mbalimbali ikiwemo kujenga uelewa wa pamoja umuhimu na namna ya kuratibu sekta ya NGOs; kujadiliiana kuhusu mchango wa NGOs kwenye Maendeleo ya Jamii ili na Sekta hii ipate utambuzi kama uliopo kwa Sekta Binafsi. 

Mbunge Lugangira alisisitiza kwamba kwa Mhe Rais Samia Suluhu Hassan kukubali kuwa Mgeni Rasmi wa Mkutano wa Mwaka wa NGOs ni ishara tosha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inatambua mchango muhimu wa Sekta hii ya NGOs kuweka mazingira wezeshi ya kufanya kazi ikiwemo kuimarisha mahusiano kati ya Sekta ya NGOs na Serikali.

Aidha, Mhe Neema Lugangira alisema kati ya wanufaika wakubwa wa fedha za miradi zitakazoingia Nchini kufuatia Ziara ya Mhe Rais Samia Suluhu Hassan alipoenda Kushiriki na Kuhutubia katika Mkutano Mkuu wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ni Sekta ya NGOs. Kwa Mfano, wakati wa Mkutano huo wa Umoja wa Mataifa, Shirika la Kimataifa ya Gates Foundation limetanganza kuwekeza zaidi ya Dola Milioni 922 kwa ajili ya Afua za Kuimarisha Lishe Bora na hapo hata sisi Agri Thamani tunaanza kujipanga kuchangamkia fursa hii maana tayari Masuala ya Lishe ni moja ya Ajenda ya Kipaumbele cha Serikali, Chama Cha Mapinduzi kupitia Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020-2025 na muhimu zaidi ni moja ya Vipaumbele vya Mhe Rais Samia Suluhu Hassan tokea akiwa Makamu wa Rais wa Tanzania.

Mbunge Lugangira alisema eneo ambalo linahitaji kuimairisha ni Uwazi na Uwajibikaji katika Sekta ya NGOs hususan inapokuja suala la Fedha za Ufadhili wa Miradi, Fedha ambazo zinapatikana kwa  kutumia jina la Tanzania. "Nasema hivi kwa sababu bado ipo changamoto ya NGOs kuwasilisha Taarifa zake za Mwaka na Taarifa za Miradi na Ufadhali kwa wakati na ili kuweza kutatua changamoto au kuimarisha utekelezaji   mashirikiano ya karibu kati ya Serikali na Sekta ya NGOs ni muhimu sana", Alimalizia.

Kupitia Hotuba ya Mhe Rais Samia Suluhu Hassan aliyoitoa katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, zipo fursa nyingi za NGOs ambazo zitaibuka kama sehemu ya utekelezaji wake hivyo Mbunge Neema Lugangira anazisihi NGOs katika maeneo husika kuanza kazi ya kuchakata baadhi ya maeneo. Kwa mfano, NGOs zinaweza kuanza kufanya Mapitio ya Sera na Sheria ili kuona namna bora ya kuziboresha ili kuweka mazingira wezeshe kwa ajili ya wanawake kupata haki ya kiuchumi, kisheria na kufikia usawa wa kijinsia.

"Jana katika Mkutano Mkuu Maalum wa Uchaguzi wa Viongozi wa ALAT Taifa, Mhe Rais Samia Suluhu Hassan alisema anataka kuona elimu na hamasa kubwa inatolewa kwa jamii kuhusu Ugonjwa wa UVIKO 19 na Chanjo ya UVIKO19 na hapa ipo fursa kubwa kwa NGOs kushirikiana na Serikali katika Kuishinda Vita hi dhidi ya Ugonjwa wa UVIKO 19", Alikumbushia Mbunge Lugangira ambaye pia ni Balozi wa UVIKO 19 Kitaifa

Mhe Neema Lugangira alihitimisha kwa kusisitiza wadau wa Sekta ya NGOs kushiriki katika Mkutano wa Mwaka wa NGOs aidha kwa kufika au kupitia njia ya Mtandao na wanaweza kujisajili kupitia www.nacongo.or.tz 

Mkutano wa Mwaka wa NGOs utafanyika katika Ukumbi wa Mkutano wa Jakaya Kikwete, Dodoma kuanzia tarehe 29 hadi 30 Septemba 2021.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post