Na Dotto Mwaibale, Ikungi Singida
NAIBU Waziri Wizara ya Madini Profesa Shukuru Manya katika hali ambayo haikutegemewa na wengi ametumia masaa mawili sawa na dakika 120 kumaliza mgogoro wa muda mrefu wa umilikaji mgodi wa uchimbaji dhahabu katika machimbo ya Kijiji cha Matongo yaliyopo wilayani Ikungi mkoani hapa.
Mgogoro huo ambao umemalizwa na Profesa Manya ulikuwa ukimuhusisha mmiliki halali wa mgodi huo Richard Lyamuya na wabia wenzake Israel Njiku na Helena Mtaturu ambaye alikuwa mlalamikaji na mmiliki wa eneo hilo la mgodi lenye ekari 70 ambalo alidai lilichukuliwa na Lyamuya bila ya kufuata taratibu kwa kumuhusisha Mtaturu na ndugu zake.
Kutoka na madai hayo Mtaturu ambaye ni mjane alimuandikia barua Waziri Wizara ya madini akidai kuwa kwa kificho bila yeye kujua mmiliki wa mgodi huo Richard Lyamuya ambaye ni mkazi wa Singida Mji alikwenda ofisi za madini Mkoa wa Singida ili apewe kibali cha kuchimba dhahabu kwenye eneo lake bila ya kushirikishwa.
Baada ya barua hiyo kufika katika wizara hiyo na kufanyiwa uchunguzi ndipo jana Naibu Waziri Wizara ya Madini Profesa Shukuru Manya alipofika kwenye mgodi huo na kufanya mkutano wa hadhara uliowahusisha wadau wa uchimbaji, Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Jerry Muro, Viongozi wa Serikali na Chama cha Mapinduzi (CCM) wananchi na wamiliki wa mgodi huo ambao baadhi yao waliweza kuelezea walivyokuwa wakielewa jinsi mmiliki wa mgodi huo alivyopata eneo hilo kwa kufuata sheria za uchimbaji wa madini kwa kumshirikisha Helena Njiku na kuweka kumbukumbu za makubaliano kwa maandishi na kutiliana saini.
Mmoja wa viongozi wa Umoja wa wachimba madini katika wilaya hiyo (SIREMA) Seleman Omari alisema mbele ya Naibu Waziri Wizara ya Madini kuwa anaujua mchakato mzima wa uanzishwaji wa mgodi huo na kuwa hakukuwa na udanganyifu wowote na wabia hao waliwekeana namna ya kulipana ambapo Mtaturu aliachiwa asilimia 40 huku Richard Lyamuya na Israel Njiku wakichukua asilimia 30 kila mmoja.
Mbali ya Omari kuyasema hayo Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Jerry Muro alisema suala hilo alilikuta ofisini kwake baada ya kusikizwa na mtangulizi wake Edward Mpogolo ambaye amehamishiwa Wilaya ya Same ambapo nyaraka zote zinaonesha umiliki wa mgodi huo ni wa watu hao watatu na tayari Serikali imekwisha wapa leseni ya uchimbaji na si vinginevyo.
Baada ya watu mbalimbali kutoa maelezo yao na kubaini kuwa Mtaturu aliandika barua ya madai ambayo sio ya kweli Naibu Waziri Profesa Manya alimwambia asirudie tena kufanya jambo hilo.
Profesa Manya alitumia nafasi hiyo kuwaomba wachimbaji hao kufanya kazi zao kwa upendo na kufuata sheria za uchimbaji.
Mkuu wa wilaya hiyo Jerry Muro aliwaomba wachimbaji hao kudumisha amani na kujikinga na magonjwa ya Corona na ukimwi kutokana na mwingiliano mkubwa wa watu katika eneo hilo.
Social Plugin