Na Costantine Mathias Maswa -Simiyu
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amekabidhi Kompyuta 10 na printa mbili kwa ajili ya wanafunzi kujifunza masomo ya Tehama huku akiwataka wakuu wa shule za sekondari katika jimbo la Maswa Magharibi lililoko wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu kuanzisha madarasa ya Kompyuta.
Waziri Ndaki ambaye pia ni Mbunge wa jimbo hilo ameyasema hayo kwa nyakati tofauti wakati akikabidhi vifaa hivyo kwa shule ya sekondari Buchambi na Badi zilizoko wilayani humo ambapo kila shule ilipatiwa kompyuta 5 na printa moja.
Amesema kuwa lengo kubwa la serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu ni kuhakikisha serikali inawajengea uwezo wanafunzi wa shule za sekondari kwa ajili ya somo la Tehama ili kuendana na kasi na mabadiliko ya kiteknolojia.
“Kitu kikubwa sisi kama serikali kwa sasa tumejipanga kuhakikisha kwamba somo hili la Tehama kwa wanafunzi linapewa kipaumbele zaidi ili kuendana na wakati wa sasa wa mabadiliko ya teknolojia," amesema Ndaki na kuongeza.
"Nina imani walimu mliosoma masomo haya ya Tehama mtaweka utaratibu mzuri ili kuhakikisha wanafunzi hawakosi fursa hii ya kujifunza kompyuta ili hata watakakwenda chuo kikuu waone kompyuta no kitu cha kawaida ma siyo kigeni kwao",alisema.
Aidha amewataka walimu wa shule hizo ambazo wamekabidhiwa vifaa hivyo kuvitunza na kuhakikisha viko salama ili viweze kuwanufaisha wanafunzi katika masomo yao.
Serikali kupitia mfuko wa Mawasiliano kwa wote (UCSAF) imekabidhi vifaa hivyo vyenye thamani ya shilingi Milioni 23.1 na kwamba shule 16 za sekondari zilizobaki katika jimbo hilo zitapatiwa vifaa hivyo baadae.
Social Plugin