NDAKI ATAKA JAMII KUWASAIDIA NA KUWATHAMINI WATU WENYE ULEMAVU


WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki (mwenye shati la madoadoa) ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi akikabidhi fimbo nyeupe, baiskeli na magongo kwa watu wenye ulemavu wilayani Maswa mkoani Simiyu.

Na Costantine Mathias Maswa.
JAMII imetakiwa kuwathamini Watu wenye Ulemavu kwa kuwawezesha kuwapatia mahitaji na misaada ya kibinadamu ili waweze kufanya shughuli ambazo zitawaingizia kipato badala ya kuwanyanyapaa.

Hayo yameelezwa leo na Waziri wa mifugo na uvuvi, Mashimba Ndaki wakati akipokea vifaa kwa ajili ya Watu wenye Ulemavu katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Maswa mkoani Simiyu vilivyotolewa na Kampuni ya Sigara nchini (TCC).

Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na baiskeli za matairi matatu 10, Fimbo nyeupe kwa ajili ya watu wenye ulemavu wa Macho 60 na Magongo 60 kwa ajili ya watu wenye ulemavu wa miguu na vyote vikiwa na thamani ya Sh Milioni 8.5

Waziri Ndaki alisema watu wenye ulemavu wamekuwa wakitengwa katika jamii kutokana na ulemavu walionao jambo ambalo si zuri kwani nao ni binadamu kama wengine hawakupenda kuwa katika hali hiyo.

Ndaki ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Maswa Magharibi alisema kuwa imefika hatua kwa watu wengine wanawaficha watu wenye ulemavu kama vile watoto na hivyo kushindwa kupata elimu jambo ambalo ni kuwanyima haki yao ya kupata elimu kama ilivyo kwa watoto wengine.

"Niwaombe wananchi wenzangu tuwajali watu wenye ulemavu,tuwawezeshe pale tunapoona umuhimu wa kufanya hivyo kulingana na mahitaji yao badala ya kuwanyanyapaa na kuwaficha kutokana na ulemavu walionao,"alisema.

Alisema kuwa ataendelea kuwapigania watu wenye ulemavu na amejizatiti kusimamia misingi ya haki zao ikiwamo kuhakikisha haki za raia wote wakiwamo wenye ulemavu katika wilaya hiyo na taifa kwa ujumla.

Pia ameishukuru kampuni ya TCC kwa kuweza kushirikiana nao kwa kulijali kundi hilo maalum la watu wenye ulemavu kwa kutoa vifaa hivyo ambavyo vitawasaidia na kuwaomba wasichoke pindi atakapokwenda tena kuwaomba misaada kwa ajili ya watu hao.

Mkuu wa wilaya ya Maswa, Aswege Kaminyoge pamoja na kumpongeza Waziri Ndaki kwa kazi kubwa anazozifanya za kuhudumia wananchi katika jimbo lake ambazo zimekuwa zikionekana ameomba na makampuni mengine ya watu binafsi pamoja na mashirika ya binafsi na serikali kujitoa katika kuhudumia kundi la watu wenye ulemavu kwani hata mtu ambaye si mlemavu anaweza kuupata wakati wowote.

“Tukumbuke kwamba kila mmoja wetu ni kama mtahiniwa katika uwezekano wa kukumbana na mazingira yatakayosababisha kupata ulemavu, tukumbuke maneno ya hekima , ‘Kabla hujafa hujaumbika’, kila mmoja wetu ni mtu mwenye ulemavu mtarajiwa,” anakumbusha Kaminyoge.

Naye Meneja Miradi ya Jamii kutoka kampuni ya Sigara nchini, Oscar Luoga alisema kuwa pamoja na msaada huo mdogo walioutoa wataendelea kusaidiana na wilaya hiyo kwa ajili ya kusaidia makundi maalum ya wananchi wakiwemo watu wenye ulemavu kwa kuwapatia miradi ya kiuchumi ili waweze kuinua vipato vyao na kuondokana na utegemezi.

Katika kukuza ustawi wa watu wenye ulemavu mipango inaendelea kuwahamasisha wanajamii juu ya haki na fursa kwa watu hao kwa nia ya kuwawezesha kujumuika na wanajamii wengine katika nyanja zote, ikiwamo kielimu ,kiuchumi na kuwawezesha kuinua hali za vipato vyao na kuondokana na utegemezi.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki (mwenye shati la madoadoa) ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi akikabidhi fimbo nyeupe, baiskeli na magongo kwa watu wenye ulemavu wilayani Maswa mkoani Simiyu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post