Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

NSEKELA ATAJWA MIONGONI MWA VIONGOZI BORA 50 WA KIBENKI BARANI AFRIKA KWA MWAKA HUU 2021

 


 

Kampuni ya kiutafiti ya Reputation Poll International LLC, imemtaja Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela kuwa miongoni mwa watendaji wakuu 50 wenye sifa nzuri kiutendaji barani Afrika kwa mwaka huu wa 2021.
 
Nsekela amefanikiwa kuwa mmoja wa watendaji wakuu wa benki barani Afrika walioonyesha weledi katika sekta ya uwekezaji na uvumbuzi wa kiteknolojia katika kipindi hiki ambacho dunia inapambana na janga la Covid-19.
 
Kampuni hiyo ya Reputation Poll International LLC, imesema iliona umuhimu wa kuwatambua viongozi katika sekta ya kibenki kwa kutambua mchango wa sekta hiyo katika jamii, kuunganisha watu na biashara pamoja na uchumi kiujumla kwa njia moja au nyingine.
 
Utafiti huo unaofanywa kila mwaka, uliweza kuangalia pia mchango wa watendaji wakuu wa mabenki 50 barani Afrika kwa kuangalia jinsi gani waliochochea au kupitia nafasi zao kufanya mapinduzi ya kisekta katika maeneo yafuatayo; ubora, Uadilifu, Uaminifu, Utaalam, Teknolojia, na urahisi wa upatikanaji wa mikopo.

“Wale waliosaidia mabenki yao kufikia mafanikio makubwa zaidi,” kampuni hiyo imesema.

Jina la Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Nsekela lilikua la kwanza katika orodha ya watendaji wakuu Afrika, na ni Mtanzania pekee aliyeorodheshwa na kampuni hiyo.

Hata hivyo hii ni mara ya pili kwa Nsekela kutambulika kimataifa kupitia uongozi wake, baada ya mwaka jana 2020 kutajwa katika jukwaa la viongozi bora na jarida la African Ledership Magazine.

Katika taarifa yao kampuni ya Reputation Poll International LLC imesema sekta ya kibenki iliathirika kwa kiasi kikubwa na janga la Covid-19 duniani, hasa kwa nchi za Kiafrika na hivyo kupelekea faida kwenye mitaji au kupungua hadi kufikia asilimia 7 mwaka 2020 kutoka asilimia 14 mwaka 2019 (McKinsley,2021).
 
Hata hivyo chini ya Nsekela Benki ya CRDB iliendelea kutengenza faida mwaka hadi mwaka. Tangu alipojiunga na benki hiyo mwaka 2018 kama mtendaji mkuu, Benki ya CRDB imekuwa ikiwekeza kwa kiasi kikubwa katika mifumo ya kidijitali, ikiwa ni moja ya vitu vilivochangia ukuaji wa faida kwa zaidi ya asilimia 87 mwaka 2019 na kufikia Sh120 bilioni kutoka Sh64.2 bilioni zilizopatikana kama faida mwaka 2018.
 
Katika miaka yake mitatu ndani ya benki hiyo, utendaji wa Benki ya CRDB umeimarika ukichochewa na mageuzi ya kimkakati. Mwaka jana benki hiyo ilivunja rekodi kwa kuongeza faida yake kwa asilimia 35 na kufikia Sh236 bilioni kutoka Sh175 bilioni za mwaka 2019. Na katika matokeo ya fedha ya nusu ya mwaka huu wa 2021 benki iliweza kuongeza faida yake kwa asilimia 26 kufikia Sh88.6 bilioni ukilinganisha na Sh70.4 bilioni zilizopatikana nusu ya mwaka jana 2020.
 
Akizungumza baada ya kuchapishwa kwa orodha hiyo Nsekela alisema ni jambo jema kuwa miongoni mwa viongozi wenye utendaji bora Afrika na akasema mafanikio hayo yamechangiwa na wateja, wadau na wafanyakazi wa Benki ya CRDB.
 
Nsekela amesema licha ya changamoto zilizoletwa na janga la Covid-19, Benki ya CRDB imeendelea kupata matokeo mazuri ya kifedha kutokana na  ukuaji mzuri wa mapato na faida.
 
“Pamoja na changamoto tulizokumbana nazo tumeweza kuboresha biashara yetu kwa kuweka mikakati madhubuti ya mabadiliko na kuchukua hatua kwa wakati,” amesema.

Uwekezaji thabiti katika mifumo ya kidijitali umewezesha zaidi ya asilimia 80 ya miamala kufanywa nje ya matawi ya benki nchini kote kwa hivyo kuongeza ujumuishaji kifedha kulingana na ajenda ya serikali.

“Tumeongeza kasi ya miradi ya kujipambanua kidijitali ili kuhakikisha kuwa tunahudumia wateja wetu kwa ufanisi wakati pia tukizingatia miongozo ya afya, ” Nsekela amesema.
 
Ameongeza, "Lengo letu ni kuendesha matumizi ya njia zetu za dijitali kama SimBanking, Internet banking na CRDB Wakala, ambazo itapunguza umuhimu wa wateja wetu kutembelea matawi.”
 
Chini ya Nsekela Benki ya CRDB imeweza kukuza biashara yake kwa kiasi kikubwa kwa kufanya uwezeshaji mkubwa kwa sekta binafsi. Benki hiyo pia imekuwa mstari wa mbele kusaidia serikali kutekeleza miradi ya kimkakati, kama vile mradi wa reli ya kisasa Standard Gauge Railway pamoja na mradi wa kufua umeme wa Nyerere Hydro-electric Power Project.
 
Tangu Oktoba 2018, wakati Nsekela alipoingia Benki yay a CRDB, benki hiyo pia imeongeza uwekezaji katika kusaida jamii kupitia miradi kama mbio za CRDB Bank Marathon ambayo mwaka huu zilikusanya nusu bilioni kutumiwa katika matibabu ya watoto katika taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete jijini Dar es Salaam na ujenzi wa kituo cha kisasa cha kupiga simu cha  Ocean Road Cancer institute, na kampeni ya ‘Pendezesha Tanzania’ iliyozinduliwa katikati ya mwaka jana ikiwa na mpango wa kupanda miti milioni moja na nusu nchini kote.
--

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com