Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi
**
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi ametoa salamu za rambirambi kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki kufuatia kifo cha Jaji Haji Omar Haji, Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar.
Kifo cha Jaji Haji Omar Haji kimetokea leo katika Hospitali Kuu ya Rufaa ya Mnazi Mmoja Jijini Zanzibar na anatarajiwa kuzikwa kesho Shakani, Wilaya ya Magharibi ‘B’ Unguja mnamo saa saba za mchana.
Katika salamu hizo za rambirambi, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa amepokea kwa mshtuko na huzuni kubwa taarifa ya kifo cha Jaji Haji Omar Haji.
Aidha, kupitia salamu hizo za rambirambi, Rais Dk. Mwinyi alimuomba Mwenyezi Mungu kuwapa moyo wa subira na uvumilivu katika kipindi hichi kigumu cha msiba, familia, marafiki, ndugu pamoja na wafanyakazi na viongozi wote wa Mahakama Kuu ya Zanzibar.
Salamu hizo ziliendelea kumuomba Mwenyezi Mungu kumpa rehma na kumjaalia makaazi mema peponi. Amin.
Marehemu Jaji Haji Omar Haji aliteuliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar mnamo Februari 01, 2021 na kuapishwa mnamo Februari 08, 2021.
Sambamba na hayo, mnamo Agosti 16, 2021 marehemu Jaji Haji Omar Haji aliteuliwa na Jaji Mkuu wa Zanzibar Jaji Omar Othman Makungu kuwa Jaji Mkaazi Pemba.