Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RAIS SAMIA AYATAKA MASHIRIKA YASIYO YA KISERIKALI KUZINGATIA MIPANGO NA VIPAUMBELE KUTEKELEZA MIRADI YA MAENDELEO

 Na Mwandishi Wetu Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ameyataka Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kuzingatia Mipango na Vipaumbele vya Kitaifa katika kutekeleza majukumu na miradi mbalimbali ya maendeleo.

Rais Samia amesema hayo leo jijini Dodoma wakati akizungumza na wawakilishi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika Mkutano wa Mwaka wa Mashirika hayo.

“Napenda kuyaelekeza Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kuwa na mpango mkakati wa Maendeleo utakaokwenda sambamba mpango wa Taifa wa miaka mitano," amesema

Ameongeza kuwa huko nyuma Mashirika mengine yalikuwa yakifanya kazi kulingana na matukio ukianzishwa mpango mazingira Mashirika yanakimbilia huko ili kushawishi fedha za wafadhili. Ni imani yangu mtajipanga upya kufanya kazi kwa ufanisi.

Aidha, ameyataka Mashirika hayo kuongeza uwazi na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao na miradi mbalimbali kwa kuzingatia tamaduni, mila na desturi za nchi.

Ameongeza kuwa Mashirika ya ndani yanatakiwa kupunguza utegemezi kwa wafadhili na wadau wa Maendeleo kutokana na mabadiliko ya Sera na Agenda za wadau hao bali waanzishe miradi ya kuwatengenezea fedha kwa kushirikiana na Serikali.

Aidha ameyataka Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kuhamasisha zoezi la Sensa likatalofanyika nchini mwaka 2022 ili Taifa liweze kujiletea Maendeleo katika sekta mbalimbali.

Kwa upande wake Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amempongeza Rais kwa uongozi wake mahiri uliowezesha Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kupata uongozi na kufanya kazi katika mazingira mazuri.

Ameongeza pia, kupitia mkutano huo Mashirika hayo yamepata semina elekezi kuhusu sheria, kanuni na miongozo hivyo ni matumaini kuwa sasa wamefahamu wanatakiwa kufanya nini.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Dkt. Lilian Badi amesema Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yatazingatia kufuata sheria, kanuni na miongozo pamoja na kushirikiana na Serikali ili kutoa mchango wenye tija nchini.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com