Samirah Yusuph,
Maswa. Mkuu wa mkoa wa simiyu David Kafulila ameitisha mikataba yote ya ujenzi wa mradi wa maji wa Nguliguli- mwamanege wilayani Maswa Mkoa wa Simiyu ulio chini ya wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini ofisini kwake ili ipitiwe upya .
Hatua hiyo imekuja baada ya kufika katika mradi huo na kukuta ufanisi wa mradi katika kuhudumia wakazi wa maeneo hayo ukiwa ni wa kusua sua licha ya kukamilika kwa zaidi ya asilimia 85.
Mradi huo wenye uwezo wa kuzalisha lita 18,000 kwa saa unathamani ya tsh 961 milioni ulianza kujengwa tangu Octoba 2019 ukitarajiwa kukamilika kwa kipindi cha miezi sita lakini haujakamilika hadi sasa.
"Kama wewe ni mtaalamu acha kabisa udanganyifu fanya kazi yako kuuma uma maneno katika usimamizi wa mradi ni kuishusha taaluma yako kwa hiyo mkataba, pamoja na mkandarasi ninawahitaji ofsini kwangu," Alisema Kafulila.
Mradi huo unatarajia kuhudumia wakazi zaidi ya 7000 katika maeneo ya mradi huku siku ya majaribio ya kusukuma maji kutoka kisimani kwenda katika katika vituo vya kuchotea maji mabomba yalipasuka mara Sita hali iliyosababisha zoezi lisifanikiwe.
Akizungumzia ujenzi wa mradi huo Meneja wa Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi na Mazingira Vijijini wilaya ya Maswa Mhandisi William Boniphace amesema kuwa kazi iliyobaki ni kujenga uzio katika vituo 21 vya kuchotea maji.
"Mtandao mzima wa bomba kwa vijiji vyote viwili ni km 24.8 kwa ujumla bomba zote za mradi zimetandazwa tayari tupo katika majaribio ya kuhakikisha maji yanafika katika vijiji vyote".
Katika hatua nyingine Kafulila ametembelea mradi wa chujio la maji katika mji wa Maswa lililo chini ya Mamlaka Ya Maji Na Usafi Wa Mazingira Maswa (Mauwasa) na kuitaka kamati ya ulinzi na usalama kulinda chanzo hicho cha maji kwa gharama zozote.
Ambapo ameitaka kamati ya ulinzi na usalama kudhibiti maswala ya siasa katika kutunza vyanzo vya maji ili wafugaji waache kutumia maeneo hayo malisho ya mifugo.
Mwisho.
Social Plugin