Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega akiwasalimia Wakinamamawanaojishughulisha na Kilimo cha zao Mwani muda mfupi baada ya kufika kutembelea kiwanda cha kuchakata zao la mwani cha Mwani Mariculture kilichopo Wilayani Kilwa, Mkoani Lindi.
Na Mbaraka Kambona,
NAIBU Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema Serikali imedhamiria kuviwezesha vikundi vya kina mama wanaojishughulisha na kilimo cha zao la Mwani ili waweze kuboresha uzalishaji wa zao hilo na kuinuka kiuchumi.
Ulega alisema hayo alipotembelea Kiwanda cha kuchakata Mwani cha Mwani Mariculture na kukutana na wakina mama wanaojishughulisha na ukulima wa mwani Wilayani Kilwa, Mkoani Lindi hivi karibuni.
Alisema katika bajeti ya mwaka huu 2021/2022 Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imetenga bajeti maalum kwa ajili ya kuviwezesha vikundi hivyo ili waweze kuboresha shughuli zao.
“Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imetenga pesa kwa ajili ya kusaidia vikundi vya kina mama wanaojishughulisha na shughuli za uvuvi na ukulima wa mwani, na kikundi chenu kitakuwa cha mwanzoni kuzipata pesa hizo,”alisema Ulega.
Aliongeza kuwa kupitia pesa hizo vikundi vitapatiwa vifaa mbalimbali vitakavyowasaidia kufanya kazi zao kwa ufanisi huku akitaja vifaa hivyo vikiwemo kamba, vichanja na mashine za kukaushia zao hilo baada ya kuvunwa ili mchanga usipoteze ubora wake.
Aidha, kuhusu changamoto ya masoko na bei ya zao hilo, Waziri Ulega aliwaelekeza wataalam kutoka wizarani na Mkurugenzi wa Wilaya ya Kilwa kuwapatia wakulima hao mbegu bora ambayo inakubalika katika soko la dunia ili wakulima hao waweze kuondokana na changamoto hizo na kukuza kipato chao.
Awali, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika cha Kilwa Masoko, Bakari Bakari alieleza kuwa changamoto kubwa wanayoipata ni uhaba wa vifaa vya kufanyia kazi zao za ukulima wa mwani, masoko na bei ndogo.
“Mheshimiwa Naibu Waziri hawa wote kina mama hapa wanalima zao la mwani lakini wakivuna wanalazimika kukaa nao ndani miezi miwili hadi mitatu ndio wauze, jambo hilo linafanya dhiki iwe palepale, tunakuomba utusaidie kupata masoko mengine ili tuweze kujikimu kimaisha,”alisema Bakari.
Naye, Msimamizi wa Kampuni ya Mwani Mariculture ambayo inanunua na kuchakata mwani, Roger Morre alisema kuwa wao wapo tayari kushirikiana na wakulima hao kupata mbegu nzuri itakayosaidia kuboresha uzalishaji wa zao hilo nchini.