SERIKALI YATOA BILIONI 52.975 KWA AJILI YA MIRADI YA MAENDELEO SINGIDA


Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msingwa akitoa taarifa ya wiki ya Serikali kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo Mkoani Singida.
Mkutano unaendelea
Mkutano unaendelea
**
Na Edina Malekela, Singida

SERIKALI imetoa shilingi Bilioni 52.975 mkoani Singida kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo barabara, elimu, afya, maji, huduma za utawala na uwezeshaji wa wananchi.


Hayo yamebainishwa na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa wakati akitoa taarifa ya wiki ya Serikali kwa waandishi wa habari mkoani Singida leo.

Alisema Serikali inaendelea kutoa huduma za kiutawala na maendeleo katika Mkoa wa Singida kama kawaida chini ya Mkuu wa Mkoa Dkt. Binilith Satano Mahenge, hali ya Mkoa ni shwari na wananchi wanaendelea na shughuli zao za uzalishaji mali bila bughudha.

Alisema katika kuimarisha ustawi wa wananchi wa Singida, Serikali inatekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kama ambavyo inafanya katika mikoa mingine hapa nchini na katika kufanikisha utekelezaji huo Serikali inahakikisha inatoa fedha kama ilivyopangwa.

Msigwa alisema kuanzia Mwezi huu wa tisa, Serikali imeleta shilingi Bilioni 2 na Milioni 275 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Vituo vya Afya 8 (Ntuntu-Ikungi, Mitundu-Itigi, Chibungwa/Sasajila-Manyoni, Ilunda-Mkalama, Iglansoni-Ikungi, Tyegelo-Iramba, Kasisiri-Iramba na Makuro-Wilayani Singida) na kukamilisha vyumba vya madarasa 22 katika shule za Sekondari. Hizi ni fedha ambazo zinakusanywa kutokana na tozo katika miamala ya simu.

Alisema kuna miradi mbalimbali ya ujenzi wa Barabara na Madaraja inayoendelea kutekelezwa na kati ya Machi na Septemba mwaka huu 2021, Serikali imeleta Singida shilingi Bilioni 21 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi na ukarabati wa barabara na madaraja.

"Mfano mmoja wapo ni ujenzi wa Daraja la Msingi (lenye urefu wa mita 100) katika barabara ya Ulemo-Gumanga-Sibiti. Ujenzi wa daraja hili utagharimu shilingi Bilioni 10.933, hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 69. Daraja hili pamoja na barabara zake unganishi zitakamilika Juni 2022,". alisema Msigwa.

Msigwa aliongeza kuwa pamoja na miradi hiyo Serikali imeanza kufanya upembuzi yakinifu na usanifu kwa ajili ya maandalizi ya ujenzi wa barabara ya Sabasaba, Sepuka na Ndago Kizaga yenye km 77.6.

Alitaja barabara nyingine kuwa ni ya mchepuo ya Singida (Singida bypass) ya kilometa 46, Barabara ya Mkalama-Gumanga-Nduguti-Iguguno ambayo ni sehemu ya barabara inayoanzia Bariadi mkoani Simiyu ambayo itaunganisha na Iguguno.

Adha Msigwa akizungumzia Mapambano dhidi ya Uviko-19 alisema
janga la ugonjwa unaosababishwa na Virusi vya Korona (Uviko-19). Serikali kupitia Viongozi wake na Wataalamu imeendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya kujikinga na ugonjwa huo na kupokea chanjo.

"Kwa kutambua changamoto ya kuhakikisha elimu dhidi ya ugonjwa huu inawafikia wananchi ipasavyo pamoja na kupata chanjo, Wiki hii Serikali imeanza kutekeleza Awamu ya Pili ya utoaji chanjo kwa kupanua uwigo wa vituo vya kutolea chanjo ya Uviko-19, tulianza na vituo 550 nchi nzima na sasa chanjo zinatolewa katika vituo vyote vinavyotoa chanjo zingine nchini. Kuna vituo zaidi ya 6,784 vinatoa chanjo na pia wataalamu wa kutoa chanjo sasa wanakwenda hadi vijijini na maeneo yote yenye mikusanyiko ya watu. Hata juzi kwenye mtanange wa Yanga na Simba, watu wamepata chanjo pale," alisema Msigwa.

Alisema kwa tulipofikia sasa, hatutaki Mtanzania aliyetayari kupata chanjo apate shida ya kwenda sehemu ya kuchanjwa. Tunaweka vituo vya chanjo kwenye vituo vya mabasi, kwenye masoko, vituo vya kupima uzito magari, Mwenge wa uhuru, tunakwenda mechi ya watani wa jadi na kila mahali ambapo tunaona pana weza kuwarahisishia watu kupata chanjo. Na hii ni kwa sababu, tumeona Watanzania wengi wapo tayari kupata chanjo lakini changamoto imekuwa kuvifikia vituo vinavyotoa chanjo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post