Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YASIKIA KILIO CHA MTATURU BUNGENI


SERIKALI imesema imejipanga kujenga shule za sekondari za wasichana kila Mkoa na nyingine 1,000 kwa kata zisizo na shule hizo ili kupunguza msongamano wa wanafunzi darasani na vikwazo hususani watoto wa kike kutembea umbali mrefu.

Aidha,imesema kabla ya kuanza kwa ujenzi huo itafanya tathimini ya maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya ujenzi wa shule za Sekondari mpya na mahitaji ya upanuzi wa Sekondari za kidato cha tano na sita ikiwa ni pamoja na Shule ya Sekondari Mungaa.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),David Silinde amesema hayo Septemba 9 bungeni wakati akijibu swali la mbunge wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu.

Katika swali lake, Mbunge huyo amehoji ni lini serikali itajenga Shule ya Sekondari ya Kidato cha Tano na Sita Mungaa ambayo ni ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoitoa kipindi cha Kampeni 2020 alipopita kwenye jimbo hilo.

Akijibu swali hilo Silinde amesema Shule 26 za wasichana zitajengwa kwa awamu kwa kila Mkoa na kwamba watafanya upanuzi wa Shule za sekondari 100 ili kupokea wanafunzi zaidi wa kidato cha tano na sita.

Amefafanua kuwa awamu ya kwanza ya ujenzi itaanza mwaka wa fedha 2021/2022 ambapo serikali imetenga jumla ya Shilingi Bilioni 220.

Katika swali la nyongeza mbunge huyo ameomba tathimini hiyo itakayofanyika ichukue umuhimu wa pekee kuhakikisha shule ya Mungaa ambayo ni kongwe inajengwa .

“Katika vikwazo mojawapo alivyoeleza ni pamoja na vikwazo kwa watoto wa kike katika shule zetu za sekondari ikiwemo shule za kata,sasa nini mkakati wa serikali kujenga hostel za kuweza kuchukua wanafunzi wote wa kike katika shule zetu ambazo zipo kwenye jimbo la Singida Mashariki.

Akijibu swali hilo Silinde amesema katika tathimini ya shule 100 wanazoenda kuzifanyia upanuzi nchi nzima ili kupokea watoto wa kidato cha tano,miongoni mwa shule itakayofanyiwa tathimini ni shule ya Mungaa.

“Moja ya mkakati wa serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ni pamoja na kujenga hostel ndio maana mwaka huu wa fedha tumetenga fedha nyingi katika kuhakikisha kwamba tunajenga hostel katika maeneo mbalimbali,nyinyi mmepitisha bajeti tunasubiri fedha zitakapotoka tutaainisha maeneo mbalimbali na tutazingatia Maeneo ya Singida Mashariki.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com