Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof. James Mdoe (mwenye suti ya kaki) akipewa maelezo na Mkurugenzi wa Kampuni ya Gongalimodel, ya jijini Arusha, Prof. Askwar Hilonga (mwenye suti ya bluu) kuhusu mafunzo ya kukuza ujuzi wa kuvuna mbolea ya Mboji hai na Mifumo ya Gesi inayotokana na kinyesi cha ng’ombe yaliyolewa na kampuni hiyo kupitia ufadhili wa Mfuko wa Kukuza Ujuzi (SDF)
Picha ya pamoja Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof. James Mdoe na maafisa wa Mamlaka ya Elimu Tanzaia(TEA) na wale wa Kampuni ya Gongalimodel ya jijini Arusha.
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof. James Mdoe, akipewa zawadi alipotembelea kikundi cha Wajasiriamali wa Kimaasai katika eneo la Mto wa Mbu, Monduli mkoani Arusha ambao wamenufaika na mafunzo yaliyofadhiliwa na Mfuko wa Kukuza Ujuzi (SDF).
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), Bi Bahati I. Geuzye akipokea zawadi kutoka kikundi cha Wajasiriamali wa Kimaasai katika eneo la Mto wa Mbu, Monduli mkoani Arusha ambao wamenufaika na mafunzo yaliyofadhiliwa na Mfuko wa Kukuza Ujuzi (SDF)
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof. James Mdoe, katika picha ya kumbukumbu na wanufaika wa mafunzo yaliyofadhiliwa na Mfuko wa Kukuza Ujuzi (SDF), Wajasiriamali wa Kimaasai katika eneo la Mto wa Mbu, Monduli mkoani Arusha wakati alipowatembelea.
*****************************
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof. James Mdoe amehimiza Taasisi zinazonufaika na ufadhili wa Serikali kupitia Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) kuhakikisha zinatumia vyema fedha za ufadhili wa mfuko huo na kunufaisha wananchi kwa kuwajengea ujuzi utakaowawezesha kuendesha shughuli za kiuchumi kama ilivyokusudiwa na Serikali.
Amesema Serikali inatoa fedha hizo kupitia Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kwa lengo la kuzijengea uwezo Taasisi zinazonufika na mfuko wa SDF ili ziweze kutoa mafunzo bora ya kuwajengea ujuzi wananchi hasa vijana ili waweze kuajiriwa au kujiajiri wenyewe na kuondokana na tatizo la ukosefu wa ajira.
Prof. Mdoe ametoa rai hiyo katika siku ya pili ya ziara yake ya kutembelea taasisi tano kati ya 81 zilizonufaika na ufadhili wa Mfuko wa Kuendeleza ujuzi, ambapo ametembelea kampuni ya Gongalimodel ya jijini Arusha iliyopata ufadhii wa SDF kwa ajili ya kutoa mafunzo ya kukuza ujuzi wa kuvuna mbolea ya Mboji hai na Mifumo ya Gesi inayotokana na kinyesi cha ng’ombe.
Kupitia ufadhli huo wa Shilingi Milioni 131 zaidi ya vijana 402 wamepatiwa mafunzo hayo ya kukuza ujuzi wa masuala ya Mboji hai na mifumo ya gesi ya kinyesi cha ng’ombe ambao baadhi ya vijana hao sasa wameanzisha kampuni za kutengenza mbolea hali na wengine sasa wana uwezo wa kujenga mifumo ya gesi na kulipwa ujira.
Aidha Naibu Katibu Mkuu huyo alitembelea mradi wa mafunzo ya kukuza ujuzi kwa wafanyakazi wa sekta ya Utalii na Ukarimu yaliyoendeshwa na Chuo cha Maendeleo ya Wananchi (FDC) cha Mto wa Mbu Wilayani Monduli, mkoani Arusha. Zaidi ya wanufaika 300 kati ya 400 wamepatiwa mafunzo kupitia ufadhili wa mradi huo ambapo zaidi ya Shilingi Milioni 120 zinatumika kupitia mradi huo.
Prof. Mdoe pia amehimiza wananchi wanaonufaika na mafunzo yanayofadhiliwa na SDF kujiunga katika vikundi ili kuwa na uwezo wa kuendesha shughuli za kiuchumi kwa ufanisi na kuwaasa kuchangamkia fursa ya mikopo inayotolewa katika Halmashauri.
Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) ni Mfuko unaolenga kuwezesha Taasisi zinazotoa mafunzo kuongeza ubora na ufanisi katika kutoa mafunzo ya ujuzi na stadi za kazi katika sekta sita za kipaumbele nchini ambazo ni Kilimo - Uchumi, Utalii na Huduma za Ukarimu, Uchukuzi, Ujenzi, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na Nishati.
Taasisi 81 zimenufaika na awamu ya pili ya Mfuko wa SDF ambapo kiasi cha Shilingi Bilioni 9.7 zinatumika katika ufadhili huo. Mamlaka ya Elimu Tanzania imepewa jukumu na kuratibu utekelezaji wa Mfuko huo.
Social Plugin