Na WAMJW – Kibaha, PWANI.
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Mhe Samia Suluhu Hassani imepitisha fedha kiasi cha Shilingi Bilioni 3 kwa ajili ya malipo kwa watumishi wa sekta ya afya waliosWayuhiriki katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa UVIKO-19.
Hayo yamesemwa jana na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel alipokuwa akizungumza na watumishi wa afya katika Hospitali ya Rufaa ya Tumbi Mkoa wa Pwani alipoenda kufanya ziara ya kikazi na kukagua hali ya utoaji huduma Hospitalini hapo.
“Watumishi hapa wamezungumzia suala la fedha zao wakati wanapambana na suala la UVIKO-19, tayari Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan ametoa Bilioni tatu kwa ajili ya watumishi waliokuwa wanadai kwa kufanya kazi mbalimbali katika kuwahudumia wagonjwa waliopata ugonjwa wa corona” amesema Dkt. Godwin Mollel.
Dkt. Mollel amesema kuwa ndani ya muda wa wiki mbili watumishi wote halali wanaopaswa kulipwa fedha hizo watakuwa wameshapata malipo yao.
Aidha katika mapambano zaidi ya ugonjwa wa corona, Dkt. Mollel amesema kuwa Serikali imetenga kiasi cha shilingi Bilioni 187 kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza chanjo za magonjwa mbalimbali ikiwemo ugonjwa wa corona.
Dkt. Mollel aliendelea kuelezea juhudi zinazoendela kufanywa na Serikali katika upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wote na kusema kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa Shilingi Bilioni 149.7 kwa ajili ya kugharamia watu masikini wasiojiweza kupata huduma za matibabu katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini.
“Tunaenda kuwa na Bima ya Afya kwa watu wote, Watanzania wanaoweza kulipia watalipa na wale wasiojiweza Mheshimiwa Rais amekwisha walipia” ameelezea zaidi Dkt. Godwin Mollel.
Dkt. Mollel amesema kwa muda wa miaka nane sasa mchakato wa kuwasilisha muswada wa Bima ya Afya kwa wote umekuwa ukikabiliwa na changamoto mbalimbali na hivyo sasa Serikali imejipanga kuwasilisha kuwa Sheria katika Mkutano wa Bunge wa Mwezi Novemba.
Naye Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Pwani Mhe. Hawa Mchafu Chakoma ameipongeza Serikali kwa juhudi inazozifanya kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata huduma bora za matibabu huku ikitilia msisitizo upatikanaji wa huduma za matibabu kwa wananchi wote kupitia Bima ya Afya.
Mhe. Hawa ametoa wito kwa watumishi wa Serikali kuboresha zaidi huduma za matibabu kwa kuzingatia utu ili pindi Bima ya Afya wa wote itakapo kuwa rasmi vituo vya kutolea huduma viendelee kupata wateja.
“Nawaasa watumishi wa Serikali kuacha kufanya kazi kwa mazoea, Bima ya Afya kwa wote itawakosesha wateja, mwananchi ana uwezo wa kuchagua pa kwenda kupata huduma za matibabu akiwa na bima hiyo hiyo aidha aende kituo cha Serikali au binafsi, hivyo tuboreshe huduma zetu zaidi” amesisitiza Mhe. Hawa Mchafu.
Mwisho.
Social Plugin