Na Mwandishi wetu, Dar
Tanzania na Ufaransa zimetajwa kuwa ni ujumbe wa utulivu, amani na maendeleo duniani na kwamba tukio la hivi karibuni katika ubalozi huo halikuathiri kwa namna yeyote mahusiano baina ya Nchi hizo.
Balozi wa Ufaransa hapa nchini mhe. Frederic Clavier ameyasema hayo Jijini Dar es Salaam alipokutana kwa mazungumzo pamoja na kumuaga Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) baada ya kumaliza muda wake wa uwakilishi hapa nchini na kuongeza kuwa katika kipindi chote cha utumishi wake ameiona Tanzania kuwa ni ujumbe wa utulivu,amani na maendeleo kwa Bara la Afrika na duniani kwa ujumla.
“Katika kipindi chote cha uwakilishi wangu hapa Tanzania, nimeiona Tanzania kuwa ni ujumbe wa utulivu, amani na maendeleo kwa Bara la Afrika na duniani kwa ujumla,” Amesema Balozi Clavier.
Balozi Clavier ameongeza kuwa ushirikiano kati ya Ufaransa na Tanzania katika nyanja mbalimbali za maendeleo ikiwemo elimu, afya, miundombinu biashara na uwekezaji umeendelea kukua kwa kiwango kikubwa na kwamba Ufaransa itaendela kukuza mahusiano hayo ya kihistoria baina ya nchi hizo mbili.
Ameongeza kuwa Ufaransa itaendelea kutoa kipaumbele katika kuendeleza uchumi wa buluu ambao kwa sasa umewekewa mikakati mahususi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kama chanzo kipya cha kuongeza mapato ya serikali lakini pia kupunguza umasikini kwa Watanzania wote na kwamba anaporejea Ufaransa atahamasisha makampuni, wawekezaji na wafanyabiashara mbalimbali kutoka Ufaransa kuja kuwekeza Tanzania.
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) amemshukuru Balozi Frederic Clavier kwa kuimarisha na kuendeleza mahusiano baina ya Tanzania na Ufaransa.
Balozi Mulamula amempa pole Balozi huyo kwa tukio la kihalifu lililotokea hivi karibuni katika Ubalozi wa Ufaransa na kumhakikishia kuwa licha ya tukio hilo ambalo lilidhibitiwa na vyombo vya dola,Tanzania ni salama.
Social Plugin