Medani ya soka nchini imepata pigo kufuatia kifo cha aliyewahi kuwa Rais Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Alhaji Muhidin Ndolanga kilichotokea leo jioni Dar es Salaam.
Ofisa habari wa TFF, Clifford Ndimbo amesema kifo cha Mzee Ndolanga kimetokea katika Hospitali ya TMJ
“Ni kweli shirikisho na familia ya mpira wa miguu tumepata pigo la kuondokewa na Mzee wetu Alhaji Muhidin Ndolanga aliyewahi kuwa Rais wa TFF kilichotokea leo katika Hospitali ya TMJ.
Kwa sasa taratibu za kuuhifadhi mwili wa Mzee wetu ndio zinaendelea hivyo taarifa rasmi kuhusu utaratibu wa mazishi zitatolewa,” alisema Ndimbo.
Ndolanga atakumbukwa kwa misimamo yake pindi alipokuwa Rais wa TFF na kabla ya hapo akiwa mwenyekiti wa kilichokuwa Chama cha Mpira wa Miguu Tanzania (FAT) kuazia 1992 hadi 2004.