Katika maegesho ya gari nchini Thailand katika mji mkuu wa Bangkok, utaona mbogamboga zikiwa zimeota katika paa ya magari ya kukodi ambayo yana rangi mbalimbali za kung’aa.
Vizuizi vikali vilivyowekwa nchini Thailand dhidi ya Covid-19 vimesababisha mji huo ambao ulikuwa na hekaheka nyingi kuwa na utulivu, na kufanya madereva wa teksi kukosa kazi.
Baada ya kukosa wateja, madereva wengi waliondoka mjini na kwenda nyumbani kwao vijijini, na kuacha kile kilichoitwa makaburi ya taksi.
Je, kazi hizi zinatokomea?
Na sasa kampuni moja imeamua kutumia paa za magari hayo ambayo hayafanyi kazi kama shamba la kulimia mbogamboga, ambapo wanatarajia wanaweza kusaidia kuwalisha madereva na wafanyakazi wengine.
Wafanyakazi wa taksi za ushirika wa Ratchaphruek wametengeneza bustani ya mbogamboga kwa kuweka udongo juu ya karatasi nyeusi za plastiki.
Wamepanda mbegu mbalimbali za mboga kama pilipili , matango na zukini. Wana matumaini kuwa baada ya kuwasaidia madereva, chakula chochote kitakachosalia kitauzwa sokoni.
Biashara ya taksi mjini Bangkok kwa kawaida inategemea utalii katika sehemu kubwa lakini marufuku yaliyowekwa ya kuzuia wageni kuingia nchini humo ina maana kuwa karibu kila kitu kimesimama.
“Hili ndilo chaguo letu la mwisho,” Thapakorn Assawalertkun, mmoja wa wamiliki wa kampuni aliwaambia wakala wa habari AFP, aliongeza kusema kuwa magari mengi yana mkopo mkubwa bado ambao hawajamaliza kulipa.
“Kuotesha mboga za majani katika paa la taksi hakutaharibu magari hayo kwa kuwa kuna mengine ambayo yameshaharibika na hayawezi kutengenezeka . Kuna ambayo yameharibika injini, hayana matairi, hakuna kitu kinaweza kufanyika,” alisema.