Mwenyekiti wa TUGHE Archie Mntambo akiongea Kwenye Mkutano wa wanawake Jijini Dodoma
Katibu mkuu wa TUGHE- Taifa Hery Mkunda
Na Dotto Kwilasa, Dodoma.
CHAMA cha wafanyakazi wa Serikali kuu na Afya (TUGHE) kimewataka viongozi watakaochaguliwa kuongoza chama hicho kwa upande wa wanawake kuwa waadilifu na kuachana na masuala ya uanaharakati.
Mwenyekiti wa Chama hicho (TUGHE) Archie Mntambo ameyasema hayo leo Jijini hapa wakati akifungua mkutano wa wanawake uliohusisha jumla ya wajumbe 110 kutoka nchi nzima kwa lengo la kuchagua viongozi .
Mntambo amesema ikiwa wanawake hao wataachana na uanaharakati itasaidia Jamii na Serikali kuwaamini hasa linapofika suala la maamuzi na kukubali kutoa ushirikiano katika masuala mbalimbali.
“Kuwa Kiongozi wa TUGHE sio uanaharakati, Serikali haitaki kiongozi mwanaharakati, hutafika hata siku moja kwenda kumshawishi Rais, Waziri na Katibu Mkuu kama wewe ni mwanaharakati,"amesema na kuongeza;
Ikitokea kiongozi wa namna hii basi hakuna mtu atakuamini,kabla hujatokea tayari wameshakukataa, tusifanye uongozi wetu Kuwa kichocheo cha chuki kwa wananchi” amesema
Kwa upande wake Katibu mkuu wa TUGHE- Taifa Hery Mkunda amesema Umoja huo uliundwa ili kutetea maslahi ya wanawake kwa mujibu wa Katiba na kwamba tayari wamewapa kipaumbele pia vijana na walemavu ambazo ni kamati changa.
"TUGHE inatarajia kuchagua viongozi wao wakuu wa kamati ya wanawake Taifa Septemba 29 baada ya waliokuwa kwenye nyadhifa hizo kumaliza muda wao wa miaka mitano,hatua hii inasaidia kwa kiasi kikubwa kuchochea nguvu Kwa wanawake,"amesema.
Mkunda ametumia nafasi hiyo kuwataka wajumbe hao kuchagua viongozi wanawake watakaokuwa wabeba maono na hoja za wanawake kwa kufanya maamuzi imara na yenye tija.
Social Plugin