Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

PROF. MKENDA SERIKALI IMEDHAMIRIA KUIMARISHA KILIMO KUTOKA KILIMO CHA KUJIKIMU NA KUWA CHA KIBIASHARA

 Waziri wa Kilimo Prof. Adolph Mkenda

Na Dotto Kwilasa - Dodoma

SERIKALI imedhamiria kuimarisha kilimo kutoka kilimo cha kujikimu  na kuwa cha kibiashara Kwa kuondoa  uhaba wa maafisa ugani ambao unaikabili sekta hiyo.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Kilimo Prof. Adolph Mkenda leo Wilayani Mpwapwa Mkoani Dodoma wakati akifungua mafunzo rejea ya kanuni bora za zao la Alizeti kwa maafisa ugani wa Tarafa na kata kutoka katika Mikoa ya Singida,Dodoma na Manyara .

Mafunzo hayo yana  lengo la kuongeza uzalishaji wa alizeti na mkakati wakuongeza kipato cha maafisa ugani katika mikoa yote nchini na nguvu kubwa itaongezwa katika mikoa inayolima kwa wingi zao la alizeti.

Akiongea kwenye uzinduzi huo amesema kwa sasa kuna uhaba wa Maafisa hao ambapo kwa sasa idadi yao ni  6704 sawa na 33%  huku mahitaji ya  maafisa hao ikiwa  ni 20,538.

"Ili kuinua kilimo tunatarajia kuboresha miundombinu ili kuzalisha mazao kwa wingi na  kukidhi mahitaji ya viwanda vya ndani na ziada kuuzwa nje ya nchi,"amesema.

 Profesa Mkenda amesema hali hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza uzalishaji wa zao la mkakati la alizeti na kuondokana  na uhaba wa mafuta ya kupikia ambao hutokea mara kwa mara.

"Hapo awali Kilimo cha alizeti nchini hakikupewa kipaumbele hali ambayo ilipelekea zao la alizeti kutokuwa na tija  na hivyo uzalishaji kushuka huku akiwataka maafisa ugani nchini kuwa na mashamba darasa ya alizeti pamoja na mashamba yao wenyewe ili yawe ya mfano ikiwa ni pamoja na  kujiongezea kipato,"amesema.

Ameongeza kuwa ,maofisa ugani walikuwa hawatumiwi ipasavyo katika kilimo na kutaka shughuli za kilimo kuangaliwa upya ili kilimo kiweze kuwa cha tija ambapo Serikali itashirikiana na Tamisemi katika kuwawezesha maofisa ugani ili kuwafikia wakulima na kuzalisha ajira  kwa vijana wahitimu kupitia kilimo.

"Kwa Mwaka wa Kilimo 2021/2022 tutahakikisha changamoto za mbegu na pembejeo za kilimo zinapatiwa ufumbuzi ili suala la kilimo liweze kufanikiwa ipasavyo pamoja na kutatua changamoto ya uhaba ya maafisa ugani,"amesema.

Awali akitoa taarifa kuhusiana na mafunzo hayo,Mkurugenzi  wa mafunzo,huduma za ugani na utafiti toka Wizara ya Kilimo,Dk Wilherm Mafuru kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo amesema kuwa mafunzo rejea ya kanuni bora ya zao la alizeti toka mikoa ya singida,Dodoma na Manyara ambayo ndiyo mikoa kielelezo katika kukuza zao la alizeti huku lengo ni kufanya mafunzo kwa mazao yote.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com