Mkuu wa Mkoa wa SingidaDkt. Binilith Mahenge akifungua mkutano wa wadau wa kujadili fursa za mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP).
Mtendaji tathmini na ufuatiliaji kutoka Shirika la Maendeleo la Petroli Tanzania (TPDC) Sefiel Msovu akielezea namna mradi utakavyotekelezwa.
Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Dorothy Mwaluko akimkaribisha Mkuu wa Mkoa kufungua mkutano huo.
Mkutano unaendelea
Na Edina Malekela, Singida.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge amewataka wananchi wa mkoa huo kuchangamkia fursa za kibiashara zinazokuja kutokana na Ujenzi wa Bomba la Mafuta linalotokea Hoima nchini Uganda hadi Chongerehani mkoani Tanga.
Akifungua mkutano huo wa wadau mkoani Singida wa kujadili fursa za mradi wa ujenzi wa Bomba la Mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) Dkt. Mahenge alisema ni wakati sasa kwa wafanya biashara kuchangamkia fursa za kibiashara ili kuboresha maisha yao na taifa kwa ujumla.
Aidha Mahenge alisema kuwa Serikali haiwezi kugawa fedha kwa kila mwananchi, isipokuwa inafungua fursa mbalimbali za kuwawezesha kwa kuziandaa ambazo wadau na wafanya biashara wanatakiwa kuzidaka na kuzitumia.
"Sasa basi kwetu sisi nikuchangamkia fursa kwani kutakuwa na kambi kubwa hapa kwetu hivyo kutakuwa na mahitaji makubwa ya nyumba za kulala ,vyakula na mahitaji mengine mbalimbali", alisema Mahenge.
Naye Mtendaji tathmini na ufuatiliaji kutoka shirika la maendeleo la Petroli Tanzania(TPDC ) Sefiel Msovu alisema kuwa mradi huo wenye jumla ya kilomita za mraba 1443. Huku kutoka Hoima hadi mpakani ni kilomita za mraba 296 na kutoka misenyi hadi Chongerehani kwa upande wa Tanzania ni kilomita za mraba 1147.
Msovu alisema kuwa mradi huo unatekelezwa kwa gharama ya shilingi Tirioni nane sawa na zaidi ya milioni mia tatu Dola za kimarekani huku kiasi cha asilimia themanini kitabaki nchini kwa sababu shughuli kubwa kwa kiwango hicho kitakuwa kinafanyika nchini.
Aliongeza kuwa kwa Mkoa wa Singida bomba hilo linapita kwenye wilaya tatu za Mkalama ,Iramba na Singida DC na katika Wilaya ya Singida DC kutajengwa kambi kubwa namba kumi na moja itakayo chukua wafanyakazi zaidi ya 1,000 ambapo itachochea zaidi kuongeza Uchumi wa Singida ikiwa wana Singida watachangamkia fursa hiyo.
"Rai yangu kwa wana Singida ni kuchangamkia fursa moja kwa moja shughuli za mradi kwanza zimetengwa kwa ajili yao vilevile katika maeneo ambayo mradi unapita wananchi wa eneo husika watakuwa wanapata kipaumbele, Sisi watekelezaji wa mradi tunawaomba wananchi wachangamkie fursa ili kukuza kipato chao", alisema Msovu.
Nao baadhi ya wananchi akiweko Ivani Kamugisha waliipongeza Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwaona zaidi wao na kuwapa kipaumbele watanzania katika ujenzi wa bomba la mafuta.
Social Plugin