Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

UNATAKIWA KULA WALAU KILO 15 ZA NYAMA KWA MWAKA



Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Amosy Zephania.

***
WIZARA ya Mifugo na Uvuvi, imesema bado ulaji wa nyama nchini ni mdogo, ukilinganisha na kiwango cha ulaji wa kilogramu 15 kwa mwaka kinachotakiwa kiafya.

Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Amosy Zephania, alisema kwa mwaka huu, Shirika la Chakula Duniani (FAO), likielekeza kila mwananchi kutumia angalau kilogramu 50 kwa mwaka, ili kupata protini inayohitajika.

Aliyasema hayo wakati akizungumza na menejimenti ya Kampuni ya Shamba la Kuku la Irvine’s Tanzania Ltd lililopo wilaya ya Siha, mkoani Kilimanjaro.

“Kutokana na mahitaji hayo, serikali inatarajia kuendelea kutoa elimu kwa Watanzania kuona umuhimu wa ulaji wa nyama. Sensa ya mifugo ya mwaka 2019/2020 inaonyesha katika kaya zinazojishughulisha na kilimo na ufugaji Tanzania ni zaidi ya milioni saba.

Kaya zaidi ya milioni nne, ambazo ni sawa na asilimia 55. 3, zinafuga kuku kuanzia 10 na kuendelea. Hii inaonyesha jinsi tunavyozungumza kuku tu, nazungumzia maisha ya Watanzania kuanzia ngazi ya chini hadi juu.”

Alisema ni wajibu wa kampuni hiyo kuhamasisha wananchi kujikita katika ufugaji wa kuku hali itakayosababisha kuwapo kwa ongezeko la ulaji wa nyama kwa Watanzania na kujipatia kipato.

Awali, Meneja Masoko na Uendelezaji wa Biashara wa Kampuni ya Irvine’s, Jeremia Kilato, alisema wanazalisha vifaranga zaidi 220,000 kwa wiki, ingawa wanatarajia kuongeza uzalishaji wa vifaranga zaidi ya 290,000, kwa wiki.

“Tunajivunia uzalishaji wa kisasa na wenye ubora wa kimataifa, lakini kwa sasa tunakabiliwa na matatizo ya ongezeko kubwa la uhitaji wa vifaranga hasa katika kipindi hiki cha ugonjwa wa UVIKO 19. Sasa kampuni imeweka mikakati ya kuweza kununua mashine mpya itakayoongeza uzalishaji huo,”alisema Kilato.

Aidha, alisema kampuni hiyo inatarajia kuendelea kusambaza vifaranga katika wilaya zote na mikoa yote, ambapo hadi sasa tayari wamesambaza katika mikoa 13.

Meneja wa Kituo cha Uwekezaji cha Kanda ya Kaskazini, Daud Riganda, alisema mwekezaji huyo yupo kihalali na yupo kwenye hatua za mwisho za kupata mkataba wa kiuwekezaji.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com