Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI Profesa Riziki Shemdoe (katikati waliokaa) akiwa kwenye picha ya pamoja na wataalamu na wadau mbalimbali wa Fedha na Ukaguzi muda mfupi baada ya kufungua kikao kazi cha kujadili matokeo ya Ukaguzi wa Hesabu za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2019/20.
Naibu Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Divisheni ya Serikali za Mitaa Benjamin Mashauri akizungumza kwenye kikao hicho.
Na Godwin Myovela, Singida.
WATAALAMU mbalimbali wa Fedha wamekutana mkoani hapa kutafuta mwarobaini wa namna ya kurekebisha na ikiwezekana kuondoa kabisa dosari zilizopelekea baadhi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini kupata hati chafu na zile za mashaka- kulingana na Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka wa Fedha 2019/20.
Imeelezwa pamoja na mambo mengine, lengo la kikao hicho ni kukubaliana na kuweka mikakati ya pamoja itakayosaidia wakaguzi na wakaguliwa kutekeleza wajibu wa kisheria kwa namna ambayo itaongeza tija na kuboresha utendaji.
Akizungumza wakati akifungua kikao kazi hicho, Katibu Mkuu TAMISEMI Profesa Riziki Shemdoe alisema matokeo ya ukaguzi huo hayakuwa ya kuridhisha kutokana na mwenendo usioridhisha wa Hati za Ukaguzi zilizopatikana ikilinganishwa na mwaka wa fedha uliotangulia wa 2018/19.
"Kumekuwa na poromoko la halmashauri kupata hati safi na hii haikubaliki. Haiwezekani kuwe na poromoko la hati safi kutoka halmashauri 176 mwaka 2018/19 hadi halmashauri 124 mwaka 2019/20...nahitaji kikao hiki kije na mkakati madhubuti na maazimio yatakayosaidia kuleta maboresho stahiki," alisema.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, halmashauri zilizopata Hati Zenye Shaka ziliongezeka kutoka 9 mwaka 2018/19 hadi halmashauri 53 mwaka 2019/20, huku 8 zikijikuta zinapata Hati Chafu.
Alisisitiza kwa kuzitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa kupitia Waweka Hazina na Maafisa Masuuli kuwa makini katika kipindi hiki wanapokwenda kufunga vitabu, kwa kuhakikisha zinajiepusha na aina yoyote ya ubadhirifu na matumizi yasiyofaa ya fedha za umma ili kuepuka hati chafu na zile zenye mashaka.
"Ni matumaini yangu baada ya kikao hiki ambacho namuona mwakilishi wa Ofisi ya CAG, Mhasibu Mkuu wa Serikali, Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Maafisa Masuuli na wadau wengine mliopo tuhakikishe tunajadili kwa kina changamoto zote zilizojitokeza na kuhakikisha hazijirudii," alisema.
Aidha, Prof. Shemdoe alisisitiza baada ya kikao hicho kilichofadhiliwa na USAID kupitia Mradi wa PS3+, Ofisi ya Rais-TAMISEMI itakuwa tayari kutekeleza makubaliano yatakayofikiwa na kuratibu utekelezaji wa yale yote yatakayopaswa kutekelezwa na Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa katika muktadha wa maboresho ya huduma bora kwa wananchi.
Kwa upande wake, Naibu Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Divisheni ya Serikali za Mitaa, Benjamin Mashauri, alibainisha sababu kubwa ya ongezeko la hati chafu na zile zenye mashaka kuwa kubwa ni changamoto kwenye eneo la uandaaji wa Hesabu.
Pia Mashauri alisema eneo lingine linalopelekea hali hiyo ni kwenye mapato ambayo pamoja na mambo mengine, mapato mengine hukusanywa lakini hayapelekwi benki wala kwenye mifumo stahiki.
Aliongeza kuwa changamoto nyingine ni kwamba taarifa za kwenye vitabu haziendani na taarifa halisi za mapato yanayokusanywa. Hali inayopelekea kiasi kikubwa cha matumizi ya Fedha za Umma kujikuta zikifanyiwa matumizi bila ya kuwa na viambatanisho stahiki.
"Vilevile kuna masuala ya changamoto za matumizi ya mifumo ya kisasa katika uandaaji wa hesabu kulingana na Kanuni za Mfumo wa Kimataifa za uandaaji wa Hesabu za Taasisi za Umma.., huko nyuma tulikuwa na mfumo wa Epicor sasa ni Muce, hivi vyote visipozingatiwa hupelekea pmatokeo ya uzalishaji huu wa hati chafu na zenye mashaka," alisema Mashauri.
Social Plugin