Dotto Mwaibale
WANAMUZIKI jijini Mwanza wamezindua Maadhimisho ya Kimataifa ya Siku ya Muziki Duniani kwa kutembelea Kisiwa cha Saanane Island lengo likiwa ni kutangaza utalii wa ndani.
Wanamuziki hao walifanya safari hiyo ya kitalii katika kisiwa hicho jana ikiwa ni moja ya shughuli kuelekea Maadhimisho ya Siku hiyo ambayo kilele chake kitakuwa ni Oktoba 1, 2021 Jijini Arusha.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanamuziki Tanzania (TAMUFO) Stella Joel alisema Wanamuziki wa kada mbalimbali katika baadhi ya mikoa wameshiriki kuzindua maadhimisho hayo katika maeneo yao kwa kuhamasisha shughuli mbalimbali za maendeleo.
Alisema kwa Dar es salaam Wanamuziki hao walikutana Makumbusho ya Taifa iliyopo Posta ambapo walikuwa na jumbe mbalimbali za Kuhamasisha maendeleo ya shughuli za kijamii pamoja na kuutangaza muziki.
Joel alisema kwa upande wa Arusha Wanamuziki walikutana katika Makumbusho ya Kihistoria ya Taifa na kupata historia mbalimbali ikiwemo ya kuanzishwa kwa Azimio la Arusha.
Alisema na kwa Mkoa wa Mwanza walitembelea kisiwa hicho cha Saanane Island.
Joel alitumia nafasi hiyo kumshukuru sana Mhifadhi wa Kisiwa hicho cha Saanane Island Kamanda Eva Mwangomo kwa kuupa heshima Umoja wa Wanamuziki Tanzania (TAMUFO) ambao umeandaa maadhimisho hayo kwa kutoa fursa ya kutembelea kisiwa hicho kwa lengo la kukitangaza na kufanya ziara hiyo ya utalii wa ndani kujionea vivutio vya utalii wa nchi yetu.