Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WATUMISHI WA TRA, WADAU WA KODI WAELIMISHWA MABADILIKO YA SHERIA ZA KODI


Afisa Msimamizi wa Kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Makao Makuu Dar es Salaam Bw. Zakeo Kowero akiwasilisha mada ya mabadiliko ya sheria za kodi ya mwaka 2021 kwa viongozi wa Vyama vya Msingi vya Ushirika pamoja na wanunuzi wa zao la pamba wa mkoani Simiyu wakati wa semina iliyoandaliwa na TRA mjini Bariadi mkoani humo.

Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Simiyu Bw. Michael Nsobi akifafanua jambo wakati wa semina ya mabadiliko ya sheria za kodi ya mwaka 2021 iliyofanyika mjini Bariadi mkoani humo.

Afisa Msimamizi Mwandamizi wa Kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Mara Bw. Zake Wilbard akifafanua jambo wakati wa semina ya mabadiliko ya sheria za kodi ya mwaka 2021 iliyofanyika mjini Bariadi mkoani Simiyu.

Mmoja wa viongozi wa Vyama vya Msingi vya Ushirika wa mkoani Simiyu akichangia hoja wakati wa semina ya mabadiliko ya sheria za kodi ya mwaka 2021 iliyoandaliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mjini Bariadi mkoani humo.
Baadhi ya viongozi wa Vyama vya Msingi vya Ushirika pamoja na wanunuzi wa zao la pamba wa mkoani Simiyu wakiwa katika semina ya mabadiliko ya sheria za kodi ya mwaka 2021 iliyoandaliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mjini Bariadi mkoani Simiyu.
(PICHA ZOTE NA TRA).

***************************

Na Mwandishi wetu

Simiyu

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inaendelea kutoa elimu ya mabadiliko ya sheria za kodi ya mwaka 2021 kwa watumishi wa mamlaka hiyo, wadau na walipakodi katika mikoa mbalimbali hapa nchini.

Akizungumza na watumishi, wadau na walipakodi hao katika mikoa ya Simiyu na Mara, Afisa Msimamizi wa Kodi kutoka TRA Makao Makuu Dar es Salaam Bw. Zakeo Kowero alisema kwamba, lengo la kutoa elimu hiyo ni kuwa na uelewa mmoja kwa watumishi wa TRA na kwa upande wa walipakodi na wadau ni kuwafahamisha mabadiliko yaliyotokea ili kuongeza uhiari wa ulipaji kodi.

“Tumeamua kuzunguka kutoa elimu hii ya mabadiliko ya sheria za kodi yaliyofanywa na Serikali katika mwaka wa fedha 2021/22 ili kuhakikisha watumishi tunakuwa na lugha moja wakati tunapowahudumia wateja wetu na kwa upande wa wadau na walipakodi ni kuwafahamisha kuhusu mabadiliko yaliyotokea,” alisema Kowero.

Kati ya mabadiliko yaliyotokea ni pamoja na kuongeza idadi ya waajiriwa kwenye Kodi ya Kuendeleza Mafunzo ya Ufundi Stadi (SDL) kutoka wafanyakazi wanne hadi kumi lakini uwasilishaji wa ritani utaendelea kama kawaida bila kujali idadi ya watumishi.

Eneo lingine lililofanyiwa mabadiliko katika kodi hii ya uendelezaji mafunzo ya ufundi stadi ni la taasisi za kidini ambapo zimesamehewa kulipa kodi kwenye huduma za afya ya umma.

“Lengo la kuongeza idadi ya waajiriwa ni kuwapunguzia mzigo waajiri wadogo ili kukuza mitaji yao na dhumuni la kutoa msamaha kwenye taasisi za dini ni kuzipa unafuu katika kutoa huduma kwa jamii,” alibainisha Kowero.

Akizungumzia mabadiliko yaliyofanyika katika Kodi ya Majengo alisema kwamba, viwango vimeongezeka kwenye nyumba za kawaida katika Majiji, Manispaa na Halmashauri za Miji kutoka shilingi 10,000 hadi shilingi 12,000 kwa mwaka.

Kwa upande wa kila sakafu ya nyumba za ghorofa katika majiji, manispaa, halmashauri za miji, kodi imeongezeka kutoka shilingi 50,000 hadi shilingi 60,000 kwa mwaka na kwa nyumba za ghorofa zilizoko katika halmashauri za wilaya, kodi imeongezeka kutoka shilingi 20,000 hadi shilingi 60,000 kwa jengo zima kwa mwaka.

“Hata hivyo, Serikali imebadilisha njia ya utozaji kodi hii ambapo kwa sasa kodi ya majengo inalipwa kupitia njia ya ununuzi wa umeme wa LUKU kwa kukata shilingi 1,000 kwa mwezi kwa nyumba za kawaida na shilingi 5,000 kwa mwezi kwa nyumba za ghorofa,” alieleza Kowero.

Kwenye Sheria ya Usajili wa Vyombo vya Moto, Serikali imepunguza kodi ya usajili wa namba binafsi kutoka shilingi 10,000,000 hadi shilingi 5,000,000 na usajili huo utadumu kwa miaka mitatu. Lengo la mabadiliko hayo ni kuwavutia watu kusajili vyombo vyao vya moto na hivyo kuongeza mapato ya serikali.

Mabadiliko mengine yamefanyika kwenye sheria ya Ushuru wa Stempu kwa mfano, ushuru wa stempu katika nyaraka mbalimbali umeongezeka kutoka shilingi 500 hadi shilingi 2000.

Naye, Danieli Singiri mmoja wa viongozi wa Vyama vya Msingi vya Ushirika wa mkoani Simiyu waliohuduria semina ya mabadiliko ya sheria mkoani humo, alisema amefurahishwa na elimu hiyo na ameiomba serikali kuangalia kifungu kipya cha kodi ya zuio ya asilimia mbili iliyowekwa kwenye mazao ya kilimo kwani kitawaumiza wakulima.

“Tumefurahi kwa kutupatia elimu hii muhimu lakini tunaiomba serikali iangalie kodi ya zuio ya asilimia mbili kwenye mazao ya kilimo kwani itawadidimiza wakulima kwasababu watapokea fedha pungufu japokuwa lengo la kodi hii ni zuri na imelenga kuongeza mapato ya serikali hata hivyo nashauri itafutwe njia nyingine tofauti na hii,” alisema Singiri.

Elimu ya mabadiliko ya sheria za kodi imekwishatolewa katika mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Singida, Tabora, Kigoma, Manyara, Arusha, Kilimanjaro na Tanga. Kwa sasa elimu hiyo inaendelea kutolewa katika mikoa ya Simiyu, Mara, Mwanza, Mbeya, Songwe, Rukwa na Katavi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com