WAZIRI wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima amezindua mfumo wa kidigitali wa usimamizi shirikishi katika utoaji wa huduma za afya (AfyaSS), ili kuwezesha upatikanaji wa taarifa sahihi na kwa wakati muafaka.
Akizindua mfumo huko jana Jijini Dodoma,Dkt. Gwajima amesema mfumo huo utasaidia kuboresha utoaji wa huduma za afya nchini na hivyo kufikia dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Akitoa ufafanuzi juu ya mfumo huo Mkuu wa Kitengo kidogo cha Usimamizi Shirikishi kutoka Wizara ya Afya Dkt. Chrisogone German amesema mfumo huo umetengenezwa ili kutatua changamoto mbalimbali zilizopo katika sekta hiyo ikiwemo uratibu kwenye usimamizi na upatikanaji wa taarifa kwa wakati.
“Awali ilikuwa ni changamoto sana kumfuatilia mtu lakini sasa imerahisisha,lakini pia itasaidia kwenye matumizi ya rasilimali, kabla ya mfumo huu tulikuwa tunatumia rasilimali nyingi lakini kwa sasa kutakuwa na uratibu mzuri,upatikanaji wa taarifa kutoka kwenye vituo katika ngazi zote utakuwepo na hivyo tutapunguza gharama katika usimamizi,”alisema.
Alisema tayari wametoa elimu kwa watu mbalimbali kuanzia ngazi ya Taifa hadi wilaya juu ya matumizi ya mfumo huo.
“Ili kurahisha ufanisi wake wamenunua vishkwambi 900 ambavyo vitagaiwa kwa wadau mbalimbali,vishwakmbi hivi tutavitoa vitatu kwa kila mkoa na kwenye halmashauri pia watapata vitatu,”alisema.
Mfumo huo umetengenezwa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI na Shirika lisilo la kiserikali la Path kupitia mradi wake wa ‘Data UsePertnership’ ambao umesaidia kuanzia hatua za awali za utengenezaji wa mfumo tangu mwaka 2017 hadi sasa.
Social Plugin