Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe.Profesa Kitila Mkumbo amekutana na kufanya mazungumzo na wadau mbalimbali kuhusu maendeleo ya Sekta ya viwanda na biashara nchini.
Waziri Mhe. Mkumbo amekutana na Balozi wa Uingereza nchini, Mhe. David Concar, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Serengeti Breweries, Mark Ocitti pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Twiga Cement, Alfonso Velez leo tarehe 17/09/2021.
Katika Mkutano wake na Bakozi Concar, wawili hao walizungumzia maandalizi ya Kongamano la Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Uingereza linalotarajiwa kufanyika mwezi Novemba mwaka huu.
Aidha, Balozi Concar amebainisha kuwa, Kongamano hilo limapata hamasa kubwa na kuwavutia wafanyabiashara na wawekezaji wengi wa Uingereza na kuahidi kuja kushiriki hapa nchini na wengine kushiriki kwa njia ya mtandao.
Balozi Concar ameongeza kuwa, hatua hiyo imefikiwa baada ya mwamko mkubwa wa kibiashara na uwekezaji uliopo nchini Tanzania katikabuongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita.
Kwa upande wake, Waziri Mkumbo amemuhakikishia Balozi huyo kuwa, maandalizi yanaendelea vizuri na wafanyabiashara wa Watanzania wana shauku kubwa kushiriki Kongamano hilo kwa lengo la kutumia fursa zilizopo na kubaini fursa mpya za ushirikiano baina ya mataifa hayo mawili hususan kuangalia namna gani bidhaa za Tanzania zinaweza kuuzwa nchini Uingereza.
Awali akikutuna na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL), Mark Ocitti, Waziri Mkumbo alitumia fursa hiyo kupokea taarifa ya uzinduzi wa mradi wa upanuzi wa kiwanda cha Sengereti Breweries Kilimanjaro ambao unatarajiwa kufanyika Septemba 23, 2021 ambapo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Kiwanda hicho kinatarajiwa kuwa na manufaa makubwa nchini ikiwemo kuongeza ajira na kuchochea kilimo cha shayiri na mazao mengine ambayo kiwanda hicho hutumia kama malighafi.
Vile vile, Waziri Mkumbo alikutana na Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Saruji cha Twiga, Alfonso Velez, na kukitaka kiwanda hicho kuongeza uzalishaji wa saruji nchini kulingana na mahitaji yanayohitajika nchini hususan katika kipindi hiki cha utekelezaji wa miradi kitaifa ya kimkakati ya kimaendeleo.