Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MAZISHI YA ASKARI POLISI ALIYEFARIKI AKISHANGILIA MECHI YA SIMBA NA YANGA KUFANYIKE KESHO



ASKARI wa Jeshi la Polisi, Kituo cha Polisi Mpwapwa mkoani Dodoma, Afande Rashid Mohamed Juma ambaye ni shabiki wa Timu ya Yanga amefariki dunia juzi Jumamosi, Septemba 25, 2021 wakati akitazama mchezo wa Simba na Yanga kwenye runinga.
Shuhuda aliyekuwa akitazama mpira na Rashid aitwaye Joseph Ndani Mutalima, Mkazi wa Mpwapwa amesema alifika pale dakika ya pili ya mchezo na hakuchukua zaidi ya dakika tano alianza kuishiwa nguvu.
“Alianza kuguna akiwa amesimama na nikamdaka baada ya kumlaza chini ndio akaendelea kuguna kama ng’ombe na kurusha mikono baadaye akaguna mara ya mwisho na kunyoosha miguu na mikono.
“Dakika chache baadaye walikuja Askari kumchukua, baadaye wakasema ameshafariki, sio kwamba amefariki baada ya goli hapana, wakati anaendelea kurusha mikono goli ndio lilikuwa linaingia,” amesema Joseph.
Mwili wa Rashid umeagwa jana Mpwapwa na kusafirishwa jana Jumapili kwenda nyumbani kwao wilayani Nkasi mkoani Rukwa kwa ajili ya mazishi. Marehemu ameacha mjane na watoto wawili na mazishi yanatarajiwa kufanyika kesho Jumanne.
Mechi ya Simba na Yanga iliisha kwa Yanga kuibuka na ushindi wa bao 1-0, bao la Yanga likifungwa na Fiston Mayele dakika ya 11 tu ya mchezo huo.
Kwa matokeo hayo Yanga walifanikiwa kutwaa taji la Ngao ya Jamii mbele ya wapinzani wao hao wa jadi katika Dimba la Mkapa jijini Dar es Salaam.

Na Mwandishi Wetu, Dodoma.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com