Kamanda wa Kikosi cha Usalama barabara mkoa wa Kagera Denice Kunyanja , akiongea na waandishi wa habari hawapo pichani baada ya kufanya ukaguzi kwenye magari ya abira
Na Ashura Jumapili, Bukoba
Jeshi la Polisi mkoa wa Kagera kitengo cha Usalama barabarani kwa kushirikiana na wakala wa barabara Mkoani humo (TANROADS) wameweka mikakati kabambe kuhakikisha suala la ajali za barabarani linapungua hususani kwenye maeneo ya barabara korofi ambayo ajali zimekuwa zikijirudia.
Taarifa hiyo imetolewa na Kamanda wa Kikosi cha Usalama barabarani mkoani Kagera (RTO), Denis Kunyanja ,wakati wa uzinduzi wa stika mkoani humo.
Kunyanja alisema mikakati hiyo imepangwa katika makundi mawili ikiwemo ya muda mrefu na mfupi na imeanza kutekelezwa katika barabara ya Kibeta hadi Nyangoye ambayo imekuwa ikikabiliwa na ajali za mara kwa mara.
Alisema miongoni mwa mikakati hiyo ni pamoja na ukaguzi wa vyombo vya usafiri katika mifumo hatarishi ya breki, usukani na tairi, gari litakaloonekana halina dosari katika mifumo hiyo litawekewa stika ambayo itaonyesha kuwa limeruhusiwa kufanya safari.
"Tunakagua mifumo hiyo kwa sababu utengenezwaji wake unatumia gharama kubwa jambo linalosababisha wamiliki wa vyombo hivyo kushindwa kuvikarabati na kupelekea magari hayo kupata ajali," alisema.
Kunyanja, alisema pia Jeshi hilo limeweka askari maeneo ya Kibeta ambao watayakagua magari yote makubwa ya mizigo na abiria kwenye mifumo hiyo mitatu kabla ya kuanza kuteremka mlima Nyangoye na yakishamaliza mzunguko wa Rwamishenyi yatasimamishwa tena na kukaguliwa na askari kabla ya kumalizia kuteremka mlima huo.
Aidha Kunyanja alisema wamekaa na Tanroads ambao wamekubaliana waongeze alama za barabarani ili kuongeza tahadhari kwa madereva na watumiaji wa barabara hiyo.
Alisema tayari Tanroads wameandika maandishi ya tahadhari katika barabara hiyo yanayowataka madereva kutembea mwendo wa polepole, kuongeza matuta yatakayopunguza mwendo kasi pamoja na kuweka mabango makubwa ya kuwatahadharisha madereva kupunguza mwendo kasi.
Alisema pia Tanroads wanaendelea na mkakati wa kutafuta fedha ili waweze kuhakikisha wanapunguza mteremko huo kwa kuchimba kina cha barabara pamoja na kutanua barabara hiyo pembeni.
"Na kwenye mzunguko wa Rwamishenye itawekwa nguzo kubwa itakayozuia magari yasiteremke chini endapo yatapata ajali maeneo hayo," alieleza.
Kunyanja, aliongeza kuwa taasisi hizo zimeendelea kushirikiana kutoa elimu ya matumizi bora ya barabara kwa watumiaji wote wa barabara wakiwemo madereva ili kupunguza sababu za kibinadamu kama vile uzembe wa kutotii sheria za barabarani unaosababisha ajali.
"Mbali na sababu za kibinadamu pia kuna sababu za kimazingira kama vile mvua kubwa zinazosababisha utelezi barabarani ambazo zinapelekea barabara kuwa na mashimo, hivyo Tanroads imehakikisha inatengeneza barabara zote korofi," alisema.
Alisema licha ya mipango yote hiyo bado mwaka huu wamefanikiwa kupunguza kiwango cha ajali kwa asilimia nne.
"Ukilinganisha takwimu za ajali mwaka 2020 na 2021 tumepunguza ajali mbili pekee ambazo ni sawa na asilimia nne tu.
Januari hadi Septemba, 2020 kulitokea ajali 29, kati ya hizo ajali 21zilisababisha vifo wakati ajali nane zilisababisha majeruhi ukilinganisha na Januari hadi Septemba 2021 kulitokea ajali 27 ambapo kati ya ajali hizo 17 zilisababisha vifo wakati ajali 10 zilisababisha majeruhi," alisema.
Kunyanja, alisema mikakati hiyo inaenda sambamba na wiki ya usalama babarani mkoani Kagera wakati maadhimisho yake kitaifa yanatarajiwa kufanyika Novemba 11 mwaka huu mkoani Arusha.