Spika wa Bunge Job Ndugai akiongea kwenye mkutano wa Asasi za kiraia unaoendelea Jijini Dodoma.
Na Dotto Kwilasa, Malunde 1 blog Dodoma.
ASASI za kiraia nchini (AZAKI) zimetakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia uadilifu na uzalendo kwa kutumia takwimu za kisayansi zitakazo saidia kuleta majawabi ya changamoto katika jamii.
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai amesema hayo leo Jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa maadhimisho ya wiki ya AZAKI na kusema kuwa ni wakati wa asasi hizo kijitathimini na kufanya kazi kwa mujibu wa Sheria zinazowaongoza na kuachana na migongano.
Amesema,iwapo asasi hizo hazitoruhusu migogoro ya wenyewe kwa wenyewe itasaidia kuleta matokeo makubwa kimaendeleo na kuongeza weledi kwa mustakabali wa taifa.
Spika Ndugai amesema,mbali na asasi hizo kutoa mchango wa maendeleo katika jamii bado kuna mambo hayaendi sawa kutokana na kutokuwa na ushirikiano na kuzitaka kuendelea kuongeza nguvu katika elimu,afya na mazingira.
"Endapo mtaendelea kuruhusu migogoro na migongano ndani ya asasi hizi itakuwa ni jambo gumu kwenu kufanikisha malengo na azma mlizojiwekea,"amesisitiza.
Mbali na hayo amezitaka AZAKI hizo kuwa na mwenendo wa kuwakosoa viongozi wa Serikali pale wanapoenda kinyume na maadili ya utumishi wa umma jambo litakalo ongeza uzalendo na uwajibikaji nchini.
"Wapongezeni viongozi wanapofanikisha mambo,lakini msisite kuwakumbusha wajibu wap wanapojisahau,hii itachichea nguvu katika maendeleo na Nina Imani tutafika tunapotaka,"amesisitiza
Kwa upande wake Jenipher Kato mwakilishi wa asasi ya Wote Sawa inayojishughulisha na utoaji elimu na kutetea wafanyakazi wa majumbani amesema kuwa katika wiki ya asasi za kiraia wanatumia kuelimisha jamii kuhusu wafanyakazi wa majumbani na kuwapa uhuru.
"Tunatoa elimu ya umuhimu wa kuwapa wafanyakazi wa ndani mikataba ili wathaminiwe,tunawataka waajiri waje wajifunze namna wanavyohitajika kuwapa thamani wafanyakazi wa ndani,"ameeleza.
Naye Rais wa AZAKI Dkt. Stigma Tenga amesema pamoja na mchango mkubwa wa Asasi hizo kwenye jamii ,bado kuna haja ya Bunge kuleta mabadiliko zaidi Kwa kupitia upya sheria ,taratibu na miongozo iliyopitwa na wakati ili kuwezesha Asasi hizo kushiriki vyema katika utekelezaji wa majukumu bila kuwepo vikwazo.
Wiki hii pamoja na mambo mengine,bado inaendelea Jijini Dodoma na kuwakutanisha wadau mbalimbali kujadili na kujifunza mambo mengi yanayofanywa na Asasi hizo kwenye jamii na kuleta mafanikio katika afya,elimu na mengineyo huku yakiwa na kaulimbiu ya "mchango wa Asasi za kiraia katika maendeleo ya nchi".