AZAKI ZATAKIWA KUWEKA MIZANIA YA MAENDELEO KWA MMOJA MMOJA

Na Dotto Kwilasa - Malunde 1 blog Dodoma

MKURUGENZI Mtendaji wa Foundation For Civil Society (FCS) Francis Kiwanga amezitaka Asasi za Kiraia(AZAKI) kutimiza majukumu yake kwa kuongeza mchango  wa maendeleo ya nchi kwa kuweka mizania ya maendeleo kwa mtu mmoja mmoja ili kuleta tija na umuhimu wake kwenye jamii.

Ameyasema hayo  leo Jijini hapa kwenye  mjadala kuhusu nini mchango wa Asasi za kiraia kwa jamii pamoja na utoaji mchango wa Msaada wa kisheria kwa jamii katika wiki ya AZAKI inayoendelea Jijini Dodoma.

Amesema , pamoja na AZAKI nyingi kufanya kazi vizuri bado hazijafikia malengo walizojiwekea hususani katika kutokomeza umaskini wa mtu mmoja mmoja kutokana na vikwazo mbalimbali hivyo kuzitaka kuwa karibu na taasisi za Serikali ili kushirikiana na kuleta tija kwa jamii.

"Hakuna Maendeleo kama  watu wetu bado ni maskini,tunataka kuona watu wanaishi maisha ya uhakika,tunataka kuona watoto wanapata elimu nzuri ,afya na maji safi hiyo ndiyo mizania ya Maendeleo,

Tunatamani kuona jamii inaondokana na umaskini kwanza ndipo maendeleo yanaonekana,Azaki zinatakiwa kuona umuhimu wa maendeleo ya watu na siyo vitu,"ameeleza.

Mbali na hayo amesema umuhimu wa Asasi hizo utaonekana kwenye jamii ikiwa  zitapambana  kuchochea  maendeleo ya watu na siyo vitu kwani tafsiri ya  maendeleo inaanza na watu  na sio vitu pekee.

"Tunaweza tukawa na majengo mazuri ya zahanati na vituo vya afya lakini watu wakiwa masikini watashindwa kufuta zile huduma Kwa kuwa hawana uwezo wa kugharamia huduma,"amesema na kuongeza;

Nataka kuwapa mfano kuna wakati nilikuwa nasafiri kutoka Bukoba kwenda Mwanza kwa basi lakini nilikutana na masoko mazuri cha kushangaza hayakuwa na watu,watafanyaje biashara wakati hawana uwezo huo,! sasa tusijivunie namba za vitu bali maendeleo ya watu", amesema Kiwanga.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa Huru la Kilimo Nchini (ANSAF), Audax Rukonge akichangia mjadala huo wa Mchango wa Azaki kwa jamii na ni nini kifanyike amesema,Asasi za kiraia zinatakiwa kujenga tabia ya kuaminiana ili kuleta mashirikiano.

Amesema, pamoja na kujenga  tabia ya kuaminiana bado Asasi hizo zinatakiwa kuwa na mawazo ya pamoja na kuwa na uwazi kwa kile wanachokifanya.

Akichangia katika mjadala huo pia amesema kuwa ili asasi ziweze kufanya vizuri ni lazima zijenge utamaduni wa kuwa na maono ya pamoja,vipaumbele vya pamoja,utekelezaji wa pamoja na kuwa na mifumo ya uwajibikaji wa  pamoja.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Anna Henga amesema wananchi  Serikali inawekeza sana lakini miradi mingi lakini  haidumu Kwa kuwa wananchi Wengi hawana mwamko wa maendeleo Kutokana na dhana ya umaskini inayowakabili.

Amesema ,wananchi wasipokuwa na uwezo hawawezi kutambua thamani ya miradi na kushindwa kuitunza.

"Tunapaswa kutumia muda wetu mwingi kiwaelewesha Wananchi kuhusu maana ya maendeleo na umuhimu wake ili nao wapate kushiriki ujenzi wa maendeleo kwa vitendo,"ameeleza.

Licha ya hayo Henga ameeleza kuwa umaskini usipo tibiwa itaendelea kuwa kidonda Kwa jamii ambapo  karibu asilimia 50 ya watoto waishio mitaani wanatokana  na ndoa zilizovunjika Kutokana na ugumu wa maisha.

"Tunataka kupambana na umaskini uliopitiliza,tunasaidia   jamii  msaada wa kisheria pale wanapokuwa wamekwama na wakati mwingine kukosa uwezo wa kumpata wakili Kwa kukosa fedha,hivyo ndivyo tunapambana walau kuiokoa jamii",amefafanua.

Pamoja na mambo mengine  ametolea mfano wa  mwanamke ambaye alitumia muda wa miaka 40 kufuatilia mgogoro wa shamba lakini baada ya yeye kuingilia kati aliweza kufanikiwa kupata haki yake ya shamba kwa muda mfupi.

"Kesi nyingi zinatumia muda mwingi nyingine zinakuwa na mazingira ya rushwa,Lazima tuokatae rushwa ,rushwa ni umaskini, tunatamani Kila mwananchi aelewe haki zake kisheria na hii itasaidia kuleta maendeleo na kumaliza kero ya kesi ndogo za kawaida kabisa zilizokuwa zikichukua miaka 2 hadi 4 kumalizika haraka,"amefafanua Mwanasheria huyo na kusema;

Tumebaini kuwa kesi nyingi ni za migogoro ya mashamba (ardhi),migogoro ya mirathi,migogoro ya ajira  na migogoro ya ndoa zilizovunjika,karibia asilimia 50 ya watoto wanaoishi mitaani wanatokana na ndoa zilizovunjika, tumekuwa tukitoa elimu kwenye mabaraza ya ndoa,kutunga sera ya mabaraza ya ndoa kwa kushirikiana na wizara husika kumaliza janga hili,"amefafanua Henga.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post