Unaweza usiamini lakini huo ndiyo ukweli, ukisikia dunia ina maajabu basi haya ni miongoni mwake. Mwanamke mmoja mkazi wa Kijiji cha Mora, Gujarat nchini India, Jivunben Rabari mwenye umri wa miaka 70, siku chache zilizopita ameushangaza ulimwengu baada ya kujifungua mtoto wake wa kwanza katika umri huo na kuingia kwenye rekodi ya kuwa miongoni mwa wanawake wachache waliokuja kupata watoto wakiwa tayari wameshazeeka.
Mwanamke huyo alifunga ndoa na mumewe, Valjibhai Rabari takribani miaka 45 iliyopita lakini kwa kipindi chote hicho, licha ya kuhangaika sana, hawakubahatika kupata mtoto katika ndoa yao.
Baada ya kuhangaika sana, hatimaye walikutana na daktari Naresh Bhanushali anayefanya kazi katika Kliniki ya Harsh IVF Centre mwanzo mwa mwaka huu na kumueleza nia yao ya kutaka mtoto.
Akizungumza na Gazeti la The National la nchini India, Daktari huyo amesema wazee hao walipofika kwake na kumueleza shida yao, aliwakatalia na kuwaeleza kwamba umri wao ulikuwa umeenda sana lakini wakasisitiza kwamba wanachokitaka ni mtoto.
Daktari huyo anazidi kueleza kwamba baada ya kuona msimamo wao bado upo vilevile, aliamua kuwasaidia na baada ya kuumiza kichwa, aliamua kujaribu njia ya kupandikiza ujauzito ambayo kitaalamu huitwa In Vitro Fertilisation (IVF).
Katika hali ambayo ilimshangaza hata daktari huyo, baada ya kukamilika kwa hatua zote za kitaalamu zilizokuwa zinatakiwa, mwanamke huyo alipata ujauzito ambao uliendelea kukua vizuri mpaka ulipotimiza miezi tisa na hatimaye akajifungua kwa njia ya upasuaji.
Akieleza tukio hilo kwa furaha, Jivunben alisema kwa miaka mingi walikuwa wakihangaika kupata mtoto na hatimaye ndoto yao hiyo imetimia, jambo ambalo wanaona ni kama muujiza kutoka kwa Mungu.
Mwanamke huyo anaeleza kwamba enzi za ujana wao, madaktari walimwambia kwamba hawezi kunasa ujauzito kutokana na matatizo aliyokuwa nayo katika mfumo wake wa uzazi.
Septemba 2019, mwanamke mwingine nchini India, Mangayamma Yaramati, naye aliushangaza ulimwengu baada ya kufanikiwa kujifungua salama watoto pacha akiwa na umri wa miaka 74, naye akitumia teknolojia ya IVF kama iliyotumika kwa wanandoa hao.
Japokuwa inafahamika kwamba wanawake wengi hufikia ukomo wa hedhi wakiwa katika umri wa kati ya miaka 40 hadi 50 na kufanya isiwezekane tena kwa wao kupata ujauzito, maendeleo ya sayansi na teknolojia ikiwemo teknolojia ya IVF, imewezesha wanawake wengi hata waliovuka katika umri wa ukomo wa hedhi, kupata watoto.
Kwa mujibu wa wataalamu, kinachofanyika katika teknolojia ya IVF, ni kutoa yai la kike kutoka kwa mwanamke, kisha kulirubitisha maabara kwa mbegu za kiume kutoka kwa mwanaume husika, kisha kiinitete kilichorutubishwa, huingizwa kitaalamu katika mji wa uzazi wa mwanamke na hatimaye, mimba huanza kukua kwa njia za kawaida na kufanikisha kupatikana kwa mtoto.
Imeandaliwa na Aziz Hashim kwa msaada wa mitandao.