AFISA Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Nicodemus Mkama amezindua wiki ya wawekezaji katika masoko ya mitaji duniani.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkama amesema CMSA inaadhimisha wiki hii ikishirikiana na wadau mbali mbali katika sekta ya masoko ya mitaji kuendesha kampeni ya kutoa elimu kwa makundi mbalimbali na umma kwa ujumla kuanzia leo Oktoba 4 hadi Oktoba 10 mwaka.
Amesema lengo kuu la kampeni hiyo ni kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu masoko ya mitaji ili kuongeza ushiriki wa wawekezaji katika masoko ya mitaji na hivyo kuchangia utekelezaji wa mpango jumuishi wa huduma za kifedha hapa nchini yaani "National Financial Inclusion Framework".
Mkama amesema kauli mbiu ya wiki hiyo ni“Mitaji Endelevu na Kulinda Maslahi ya Wawekezaji Katika Masoko ya Mitaji”
Amesema wiki ya wawekezaji duniani inaadhimishwa kimataifa ikiratibiwa na Taasisi ya Ushirikiano wa Mamlaka za Usimamizi wa Masoko ya Mitaji Duniani yaani International Organization of Securities Commission (IOSCO). Pamoja na majukumu mengine, IOSCO imeweka kanuni zenye vigezo vya kimataifa vya ushiriki na usimamizi wa masoko ya mitaji duniani ili kuwezesha nchi mbali mbali kusimamia na kuratibu sekta ya masoko ya mitaji, kwa lengo la kuepusha athari za utandawazi kwa kuzingatia vigezo vya kimataifa na ushirikiano kati ya nchi wanachama.
"IOSCO kwa kushirikiana na Mamlaka za usimamizi wa Masoko ya Mitaji, inaratibu shughuli za Wiki ya Uwekezaji Duniani kwa lengo la kuongeza uelewa na ushiriki wa wawekezaji katika masoko ya mitaji. Kushiriki katika shughuli za wiki ya uwekezaji kunawezesha wadau mbali mbali katika sekta ya masoko ya mitaji kufanya kazi kwa pamoja katika nchi zao na kimataifa.
Shughuli zitakazofanyika katika wiki hii zitajumuisha kutoa elimu kwa wawekezaji na wananchi umuhimu wa masoko ya mitaji katika uchumi, bidhaa za uwekezaji, namna ya kupata mitaji, jinsi ya kushiriki kuwekeza katika masoko ya mitaji. Hali kadhalika program hii inalenga kuongeza bidhaa za kuwekeza na kuongeza matumizi ya sekta ya masoko ya mitaji katika upatikanaji wa mitaji kwa shughuli za uchumi na kupanua wigo wa wawekezaji," Amesema Mkama.
Amesema kampeni hii ni sehemu ya utekelezaji wa mpango mkakati wa CMSA wa miaka mitano 2018/19 – 2022/23 ambao pamoja na mambo mengine unapanga kuendeleza sekta ya masoko ya mitaji Tanzania ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya masoko ya mitaji na dhamana kwa makundi mbalimbali na hivyo kuchangia utekelezaji wa Mpango wa tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22–2025/26 wenye dhima ya “Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu”
Aidha, kampeni hii inachangia utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, yenye lengo la kuhakikisha kuwa sekta ya fedha inawezesha upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu.
Muwakilishi wa Kampuni ya UTT- AMIS Pamella Nchimbi akizungumza mbele ya Wageni waalikwa wakiwemo Waandishi wa habari akieleza namna watakavyoshiriki wiki ya wawekezaji katika masoko ya mitaji duniani
Muwakilishi kutoka Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) Ibrahim Mshindo akizungumza mbele ya Wageni waalikwa wakiwemo Waandishi wa habari akieleza namna watakavyoshiriki wiki ya wawekezaji katika masoko ya mitaji duniani
Picha mbalimbali za pamoja mara baada ya uzinduzi wa wiki ya wawekezaji katika masoko ya mitaji duniani
Baadhi ya wadau mbalimbali walioshiriki kwenye hafla hiyo fupi ya uzinduzi wa wiki ya wawekezaji katika masoko ya mitaji duniani iliofanyika leo jijini Dar es Salaam
Social Plugin