Waziri wa elimu,Sayansi na Teknolojia Joyce Ndalichako akiongea na vyombo vya habari kuhusu masuala mbalimbali ya elimu Jijini Dodoma.
Na Zena Chitwanga,Dodoma
SERIKALI imewaagiza watendaji wa Wizara na taasisi zitakazotekeleza miradi ya fedha za mpango wa maendeleo kwa ustawi wa taifa na mapambano dhidi ya Uviko 19 kukamilisha mpango na maandalizi ya utekelezaji wa miradi hiyo ifikapo Octoba 30, 2021.
Hayo yamebainishwa leo jijini Dodoma na Waziri wa elimu,Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako wakati akiongea na waandishi wa habari kuhusu mchanganuo wa fedha zitakazotekeleza miradi ambayo ipo chini ya Wizara hiyo huku akibainisha sekta ya Elimu imetengewa bilioni 368.9 ambapo Wizara hiyo imepata shilingi bilioni 64.9 kutekeleza miradi iliyo chini ya Wizara hiyo.
Prof. Ndalichako amesema hadi ifikapo Oktoba 30, 2021 kila taasisi itakayotekeleza mradi huo iwe imekamilisha maandalizi na mipango ya utekelezaji ikiwa ni pamoja na kuandaa mpango kazi utakao ainisha hatua mbalimbali na taratibu za manunuzi ya huduma na vifaa.
"Ni lazima matokeo ya utekelezaji wa miradi yaendane na thamani ya fedha zilizotolewa,"amesema.
Ili kuleta mafanikio zaidi, Prof. Ndalichako amemuagiza Katibu mkuu wa Wizara hiyo kuandaa mfumo wa uratibu, usimamizi na ufuatiliaji wa miradi utakaowezesha kubaini changamoto zitakazo kuwa zikijitokeza na kuchukua hatua stahiki na kwa wakati.
"Tunataka mafanikio zaidi kupitia fedha hii,Katibu Mkuu hakikisha unaweka usimamizi wa kutosha ili tufikie malengo kwa wakati,"amesema.
Ameeleza kuwa fedha hizo zitakwenda kuimarisha ufundishaji kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu ambapo shilingi bilioni 1.47 zimetengwa, kuimarisha elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi.
"Tunataka kuongeza kiwango cha elimu ,Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 57.98 kuimarisha mazingira ya utoaji elimu ya ualimu ,"ameeleza.