Na Dotto Kwilasa,Dodoma
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Dodoma imedhibiti na kuokoa fedha na vifaa vyenye jumla ya shilingi Milioni 47.8 ambapo kati yake ni vifaa vyenye thamani ya shilingi Milioni. 41,8 vilivyochepushwa kutoka kwenye mradi wa ujenzi wa hospitali moja.
Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)Mkoa wa Dodoma Sosthenes Kibwengo amesema hayo leo Jijini Dodoma wakati akiongea na vyombo vya habari.
Ameeleza kuwa hatua hiyo imetokana na ukaguzi wa miradi 17 ya sekta ya elimu,afya na kilimo iliyolenga kuhakikisha fedha za umma zinazoelekezwa kwenye miradi mbalimbali zinatumika kwa ufanisi na uaminifu.
Amesema,katika kuhakikisha thamani halisi ya fedha inapatikana,Taasisi hiyo kwa kushirikiana na Wakala wa barabara za vijijini na mijini (TARURA) na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) inaendelea kuelekeza nguvu katika kufuatilia utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa barabara na maji kwa kuzia vitendo vya rushwa na kufanya utambuzi wa mianya ya rushwa unaolenga kutoa ushauri wa namna ya kuziba mianya hiyo.
Kwa kutambua umuhimu huo,Kibwengo amesema Agosti mwaka huu TARURA Mkoa wa Dodoma ilisaini mikataba 43 na makandarasi mbalimbali kwa kazi ya ujenzi wa barabara katika Wilaya zote za Mkoa wa Dodoma zenye thamani ya jumla ya shilingi Bilioni 10.2 ikiwa ni miradi ya awamu ya kwanza itakayotekelezwa kwa mwaka 2021/2022.
“RUWASA iligawanya mabomba yenye urefu wa mita 35,232 katika Wilaya zote za Dodoma kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa mpango wa malipo kwa matokeo awamu ya nne ambapo gharama za ulazaji wa mabomba hayo zinakadiriwa kuwa zaidi ya shilingi Ml.95”, amefafanua Mkuu huyo wa TAKUKURU Mkoa wa Dodoma.
Sambamba na hayo ameeleza kuwa katika kipindi cha robo iliyoisha jumla ya taarifa 120 zimepokelewa na Taasisi hiyo ambapo taarifa za rushwa zilikuwa 76 huku taarifa 6 kati aya hizo zikihamishiwa idara nyingine .
“Uchunguzi wa majalada 10 ulikamilika na mashauri 9 yakafunguliwa mahakamani ambapo mashauri sita yalitolewa hukumu na Jamhuri imeshinda mashauri matatu na kushindwa matatu”,amesema.
Pamoja na hayo Kibwengo ameeleza kuwa katika robo ya Oktoba hadi Disemba mwaka huu TAKUKURU itatumia mbinu ya kuwashirikishwa vijana katika mapambano dhidi ya rushwa kupitia ushirika wa UTATU WA TAKUKURU,Chama cha Skauti Tanzania pamoja na Idara ya elimu kwa kuwaelimisha kuhusu mbinu na umuhimu wa kushiriki katika kuzuia rushwa ili nao wafikishe elimu nyumbani na jamii kwa ujumla wake.
“Kazi yetu ni kuhakikisha jamii inakuwa salama dhidi ya vitendo vya rushwa,tunaendeleza mapambao kupitia programu yetu ya TAKUKURU INAYOTEMBEA kwa kufuata wananchi na kusikiliza kero zao zinazohusiana na rushwa na kuzitafutia ufumbuzi ,vilevile tutaendelea na jukumu la kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika mkoa wetu,”ameeleza.