Siku chache zilizopita, tukio lisilo la kawaida lilitokea nchini Liberia na kuzua gumzo kubwa kwenye mitandao ya kijamii.
Lilikuwa ni tukio la kijana mdogo, Emmanuel Tuloe ambaye ni dereva wa bodaboda katika Mji wa Nimba nchini Liberia, kuokota kitita cha dola za Kimarekani 50,000, sawa na takribani shilingi milioni 115 za Kitanzania zilizokuwa zimeangushwa kando ya barabara.
Katika hali ya kushangaza, kijana huyo alirudisha fedha hizo kwa mwenyewe na kusababisha watu wengi wamcheke na kumuona hana akili timamu, yaani uokote shilingi milioni 115 halafu umrudishie mwenyewe, hakika kijana huyo alionekana kuwa kilaza kupitiliza.
Tukio hilo lilivyokuwa, ni kwamba kijana huyo akiwa katika shughuli zake za bodaboda, akitokea katika eneo la Tappita kurejea nyumbani kwake alishtuka baada ya kuona maburungutu ya fedha yaliyokuwa yamefungwa kwenye mfuko wa plastiki, yakiwa kando ya barabara.
Alichokifanya, ilikuwa ni kuchukua fedha hizo na kwenda kuzihifadhi kwa shangazi yake na kumueleza kila kitu, akamwambia shangazi yake huyo kwamba anasubiri kusikia kama mtu yeyote atalalamika kupoteza kiasi hicho cha fedha, basi atamrudishia.
Muda mfupi baadaye, mwanamama mfanyabiashara, Musu Yancy alisikika katika kituo kimoja cha redio, akiwa analia na kueleza kuwa amepoteza kiasi hicho cha fedha na kuomba kama kuna yeyote aliyeokota, basi anaomba amrudishie!
Ni hapo ndipo kijana huyo alipochukua mawasiliano yake na hatimaye, akamrudishia mzigo wake wote, bila kupunguza hata senti tano!
Wema wake ulimsababishia matatizo makubwa kwani alianza kudhihakiwa na kutukanwa mno kwenye mitandao ya kijamii.
Sasa habari mpya ni kwamba, kufuatia kitendo hicho cha uungwana uliopitiliza kilichofanywa na kijana huyo, Rais wa nchi hiyo, George Weah ameguswa mno na moyo wa kipekee wa kijana huyo na kuamua kumuita ikulu jijini Monrovia.
Akiwa ikulu, Rais Weah kwanza alitaka kujua historia yake ambapo kijana huyo alimueleza kwamba alikuwa bado mwanafunzi lakini kutokana na ukosefu wa ada, aliamua kusimama masomo na badala yake, akawa anaazima bodaboda kutoka kwa moja ya marafiki zake na kufanya kazi ili akusanye fedha ambazo atazitumia kwa ajili ya ada.
Maelezo hayo yakamgusa mno Rais Weah ambaye baadaye alimtunuku kijana huyo medali ya heshima kutoka ikulu, Liberia’s Highest Orders of Distinction, akampa zawadi ya dola elfu 10, sawa na takribani shilingi milioni 23, akamnunulia bodaboda mpya mbili na kubwa zaidi, akamuahidi kwamba Rais atamgharamia ada ya masomo mpaka atakapofika chuo kikuu, ngazi ya digrii ya pili, masters.
Kama hiyo haitoshi, mwanamke aliyeokotewa fedha zake, yeye ametoa kiasi cha dola 2500, sawa na takribani shilingi milioni tano, huku Baraza la Maaskofu nchini humo Liberia Council of Churches (LCC) kupitia kwa kiongozi wake, Bishop Kortu K. Brown nalo likitoa kiasi cha dola efu 10, sawa na shilingi milioni 23.
Pia Rais Weah ameamuahidi kijana huyo kwamba atakuwa balozi wa kupinga rushwa nchini humo na atakuwa akipewa mshahara kila mwezi.
Kwa kifupi ni kwamba jamaa amepewa takribani shilingi milioni 50 za Kitanzania, pikipiki mbili na ofa ya kusomeshwa mpaka chuo kikuu lakini pia akiingia kwenye rekodi ya watu waliowahi kupewa medali ya heshima kutoka kwa rais!
Vipi, bado huamini kama wema unalipa? Bado unamchukulia kijana huyo kama kilaza? Unaambiwa malipo ni hapahapa duniani, ukifanya wema utalipwa wema, ukifanya ubaya, vivyo hivyo utalipwa ubaya!
Imeandaliwa na Hashim Aziz