Mnyama fisi
Diwani wa kata ya Kitangili Mhe. Mariam Nyangaka
Afisa Misitu wa Halmashauri ya Manispaa James Mduma
Na Mapuli Misalaba, Shinyanga
Wakazi wa Kata ya Kitangiri katika Manispaa ya Shinyanga wamewaomba viongozi wa ngazi zote kuchukua hatua za haraka za kukabiliana na matukio ya Fisi kushambulia na kuua watoto.
Wameyasema hayo leo wakati wa maombolezo ya kifo cha mtoto Albert Shija mwenye umri wa miaka 2 na miezi 10 aliyeuawa kwa kushambuliwa na fisi Jumamosi Oktoba 16,2021 majira ya saa moja usiku katika mtaa wa Imalilo kata ya Kitangili Manispaa ya Shinyanga.
Wananchi hao wamesema matukio ya watoto kuuawa na Fisi yameongezeka hali inayosababisha hofu na taharuki kubwa kwa wakazi hao ambao wameomba mamlaka husika zichukue hatua za haraka ili kukabiliana na hali hiyo inayotishia usalama huku matukio hayo yakihusishwa pia na imani za kishirikina na uzembe wa Idara husika kuzuia fisi kuzagaa mtaani.
Tukio la mtoto Albert Shija kufariki dunia kwa kushambuliwa na fisi limetokea siku chache tu baada ya mtoto mwingine aitwaye Raphael Juma Dotto mwenye umri wa miaka mitatu kufariki dunia baada ya kushambuliwa na mnyama Fisi wakati akicheza nyumba ya jirani na watoto wenzake katika mtaa wa Majengo Mapya kata ya Kitangili Manispaa ya Shinyanga Jumamosi Septemba 25,2021 majira ya saa moja usiku.
Diwani wa kata ya Kitangili Mhe. Mariam Nyangaka amekiri kuwepo kwa taharuki inayosababishwa na matukio hayo ambapo ameeleza kuwa ameitisha kikao maalumu kitakachohusisha makundi mbalimbali ya wadau watakaojadili jinsi ya kutatua changamoto hiyo.
“Hatua za moja kwa moja ni kwamba kesho tunakutana na wazee maarufu, viongozi wa dini, wazee wa mila tutawashirikisha kila nzengo tutakutana nao tujaribu kuangalia namna ya kutatua suala hili tunafanyaje ili wananchi wakae kwa amani”,amesema.
Diwani huyo ametoa wito kwa wananchi wa Kata ya Kitangili kuchukua tahadhari ya kuwalinda watoto dhidi ya mazingira hatarishi ili kuwaepusha na matukio ya aina hiyo.
“Wazazi tuwe makini kuwalinda watoto watoto wetu hasa muda wa jioni kuanzia Saa kumi na mbili mzazi uhakikishe mtoto yupo nyumban lakini pia wazazi wawe na namba za simu za viongozi kingine wananchi wawe na vitendea kazi mfano vipenga au panga vitu ambavyo wataweza kujihami",amesema
Kwa upande wa Idara ya maliasili, misitu na nyuki ya Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kwa kushirikiana na mamlaka ya usimamizi wa wanyamapori Tanzania TAWA Kanda ya Mwanza wameanza Oparesheni malumu ya kuwasaka wanyamapori aina ya Fisi ili kuthibiti matukio ya vifo na majeruhi.
Akizungumza Afisa misitu wa Halmashauri ya Manispaa James Mduma amesema kuwa operation hiyo imeanza kufuatia mfululizo wa matukio ya Fisi kujeruhi na kuua katika maeneombalimbali ya Manispaa ya Shinyanga ikiwemo kata ya Kitangili.
Mduma amefafanua zaidi kuwa utekelezaji wa oparesheni hiyo unafanyika kwa kushirikiana na maafisa wa mamlaka ya usimamizi wa wanyamapori Tanzania TAWA kanda ya Mwanza.
"Naamini tunaweza tukafanya vizuri tukishirikiana na taasisi ya wanyamapori TAWA tumekwisha kuwa na mawasiliano nao lakini kwa matukio haya mawili wamekuja na hata sasa tukonao wanaendelea na Operesheni kwa maana ya kwamba tuwasake hao fisi wanaofanya hayo matukio kwa hiyo tukishirikiana na ofisi ya wanyamapori litadhibitiwa na ndiyo maana tunafanya kazi kwa kurikiana nao vizuri",amesema.
Akizungumzia suala hilo Afisa Mhifadhi wanyamapori Daraja la Pili kutoka kikosi dhidi ya ujangili, Mwanza Mohamed Mpoto ambaye ni mmoja kati ya Askari wanaoendesha msako dhidi ya Fisi amefafanua kuhusu sheria ya wanyamapori inayohusisha madhara yatokanayo na mazingira hatarishi ya wanyama wakali.
"Mamlaka ya wasimamizi wa wanyamapori Tanzania kupitia mkurugenzi wa idara ya wanyamapori sheria namba tano (5) ya mwaka 2009 ya wanyamapori imeainisha wanyamapori wakali na waharifu na moja wapo ni fisi kwa kulitambua hilo sheria imeainisha madhara ambayo atasababishiwa mwananchi aidha kuuawa au kujeruhiwa Kuna kifuta machozi kwa kifo inatolewa shilingi Milioni moja, majeruhi shilingi laki tano, g'ombe mmoja ni shilingi elfu hamsini lakini Mbuzi ni shilingi elfu ishilini na tano (25,000)",amesema.
Oparesheni hiyo inayoendelea katika Manispaa ya Shinyanga inafuatia kukithiri kwa matukio ya kuuawa na kujeruhiwa kwa wananchi hasa watoto wadogo katika maeneo mbalimbali katika kipindi cha mwaka huu 2021.