Vifaa ya uganga
Mchawi Mkuu wa Serikali ya New Zealand, Ian Brackenbury Channell ambaye ndiye mchawi pekee duniani aliyekuwa akilipwa mshahara na serikali, amefukuzwa kazi kufuatia matamshi yake aliyoyatoa ambayo yanadaiwa kuwadhalilisha wanawake.
Brackenbury mwenye umri wa miaka 88 aliajiriwa na manispaa ya Jiji la Christchurch nchini New Zealand tangu mwaka 1998 ambapo alikuwa akishughulika na shughuli zote za kichawi katika jiji hilo, huku akilipwa mshahara mnono wa takribani dola 16,000 za Kimarekani kwa mwaka ambazo ni sawa na shilingi milioni 36.8 za Kitanzania.
Miongoni mwa kazi za kichawi zilizompatia umaarufu mkubwa, ni pamoja na kuita mvua kipindi cha ukame, kuzifanyia ndumba timu mbalimbali za nchini New Zealand ili zishinde kwenye mechi, kuikinga jamii na majanga mbalimbali pamoja na kuwa kivutio kikubwa cha utalii.
Mara kwa mara, Brackenbury amekuwa akifanya maonesho ya kitamaduni kwenye Viwanja vya Cathedral Square katika Mji wa Christchurch na kuvutia mamia ya watazamaji ambao walikuwa wakifika kumtazama akionesha utaalamu wake wa ndumba.
Kwa mujibu wa Gazeti la The Guardian la nchini Uingereza, mshahara wa mwezi Desemba, mwaka huu, ndiyo utakuwa wa mwisho kwa mchawi huyo baada ya mamlaka za serikali kukasirishwa na matamshi yake ambayo amekuwa akiyatoa katika siku za hivi karibu, yakionesha kuwadhalilisha wanawake.
Miongoni mwa matukio atakayokumbukwa nayo, ni tukio la mwaka 1988 ambapo aliitwa katika Mji wa Waimate ambao ulikuwa umekumbwa na ukame mkali wa muda mrefu. Alipofika katika mji wake, alianza kufanya ndumba zake na nusu saa tu baada ya kumaliza kazi yake, mvua kubwa ilianza kunyesha na mji huo haujawahi tena kukumbwa na ukame tangu kipindi hicho.
Katika mahojiano aliyowahi kuyafanya na chombo kimoja cha habari nchini humo, Brackenbury alieleza kwamba hataki tena kuendelea kuzichawia timu za mchezo maarufu nchini humo wa Rugby (Ragbi) ili zishinde na hiyo ilikuwa ni baada ya siku moja kukosea masharti na kusababisha timu pinzani ishinde, jambo ambalo alidai linamharibia taswira yake katika jamii.
Tukio jingine ni pale alipoitwa na Serikali ya Australia kwenda katika mji wa Outback kuombea mvua baada ya mji huo kukumbwa na ukame wa muda mrefu. Baada ya kufika eneo la tukio, kama kawaida yake alianza kufanya ndumba zake na muda mfupi baadaye, mvua kubwa ilianza kunyesha na mji huo haujawahi kukumbwa na ukame tena.
Historia inaonesha kwamba Brackenbury alizaliwa jijini London na kupata elimu yake nchini Uingereza, kabla ya baadaye kuhamia ncbhini Australia ambapo alipata kazi ya kufundisha katika Chuo Kikuu cha New South Wales kilichopo Sydney nchini humo.
Akiwa chuoni hapo, aliendelea kujielimisha kuhusu masuala mbalimbali ya kichawi na miujiza aliyokuwa anaifanya, ilimfanya mkuu wa chuo hicho kumtangaza kuwa mchawi mkuu wa chuo mwaka 1969.
Mwaka 1972 alihamia nchini New Zealand na kuweka makazi katika Mji wa Christchurch ambako alituma maombi serikalini akitaka aajiriwe kama mchawi mkuu na kulipwa mshahara, jambo ambalo awali lilikataliwa na serikali ya New Zealand.
Baada ya ombi lake hilo kukataliwa, aliendelea na maonesho ya mitaani, akiwafanyia watu miujiza ya kichawi na wengine kuwasaidia katika matatizo mbalimbali yaliyokuwa yakiwasumbua.
Mwaka 1986 aliingia matatizoni na serikali baada ya kukataa kuhesabiwa katika sensa ya watu na makazi kwa maelezo kwamba yeye hakuwa binadamu kwa hiyo hayupo tayari kuhesabiwa sawa na wakazi wengine wa mji huo.
Serikali ilikasirishwa na msimamo wake huo na kuamua kumtimua nchini humo lakini alipoondoka, wakazi wa Mji wa Christchurch walianza maandamano ya kuishinikiza serikali kumrudisha.
Baada ya maandanamo kuwa makubwa, serikali ilisalimu amri na kumrudisha katika mji huo, akaendelea na shughuli zake za kichawi ambapo mwaka 1990, Waziri Mkuu wa New Zealand kwa wakati huo, Mike Moore alimtangaza kuwa mchawi mkuu wa serikali. Alianza rasmi kulipwa mshahara mwaka 1998.
Mwaka 2009, Brackenbury alitunukiwa medali ya heshima na Malkia Elizaberth wa II kwa kuitumikia vyema jamii na kuisaidia kutatua matatizo mbalimbali yaliyokuwa yakiikabili, ikiwemo ukame na majanga ya asili.
Kufuatia uamuzi wa kufukuzwa kazi, Brackenbury amekaririwa akisema hajafurahishwa na hatua hiyo ya serikali, na sasa wasiwasi mkubwa wa wananchi wa New Zealand ni kwamba anaweza kuanza kuwaroga viongozi waliosababisha afukuzwe kazi! Ama kwa hakika dunia ina mambo!