Maelfu ya wanawake wameandamana katika miji kadhaa nchini Marekani kupinga kampeni ya kihafidhina inayolenga kudhibiti au kuzuia huduma za kutoa mimba.
Mjini Washington, takriban waandamanaji 10,000 walijitokeza karibu na ikulu (White House), kabla ya kuelekea katika majengo ya mahakama ya juu ambayo itatoa uamuzi wa mwisho kuhusu suala hilo lenye utata.
Waandamanaji walibeba mabango yenye maneno kama, Halalisha uavyaji mimba na pia mwili wangu, chaguo langu.
Suala hilo limekuwa tete zaidi tangu Septemba mosi wakati jimbo la Texas lilipopitisha sheria ya kupiga marufuku utoaji wa mimba, hatua iliyoanzisha upinzani mkali bungeni.
Siku mbili tu kabla ya mahakama ya juu kuanza kushughulikia kesi hiyo, kumekuwa na maandamano katika zaidi miji 600.