Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Ugonjwa wa UVIKO-19 umesababisha madhara makubwa kwa watanzania. Athari za ugonjwa huu ni pamoja na vifo, gharama za matibabu, pamoja na kudorora kwa shughuli za kiuchumj. Bahati mbaya, UVIKO-19 hauna dawa mpaka sasa. Njia pekee ya kudhibiti kusambaa kwa maambukizi ya ugonjwa huu ni chanjo zilizogunduliwa na kuthibitishwa na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO). Kwa mujibu wa WHO na Wizara ya Afya ya Tanzania, chanjo hizi zina uwezo wa kuwakinga watu dhidi ya kupata homa kali na kifo.
Katika kuwalinda raia wake dhidi ya ugonjwa huu, Serikali imefanikisha upatikanaji wa dozi zaidi ya milioni moja za chanjo ya UVIKO-19 ya Jensen Jensen ambazo tayari zimetolewa kwa na kutumika. Kwa sasa, dozi Zaidi ya milioni moja za chanjo aina ya Sinopharm zimesambazwa na kutolewa kwa wananchi nchi nzima.
Hata hivyo, pamoja na faida za chanjo hizi, bado kumekuwepo na upinzani miongoni mwa watanzania unaozorotesha utekelezaji wa chanjo hizi.
Moja ya changamoto kubwa inayochangia mwamko mdogo wa raia kujitokeza kuchanjwa ni kusambaa kwa taarifa, imani na dhana potofu kuhusiana na chanjo ya UVIKO-19 nchini.
Mitandao ya kijamii imechangia kwa kiasi kikubwa upotoshaji huu. Ingawa kwa upande mwingine mitandao hii imeongeza uhuru wa watu kupata na kutoa taarifa, imekuwa chanzo cha upotoshaji kuhusu chanjo.
Upotoshaji huu umejenga na/au kuongeza hofu isiyo na mashiko kisayansi katika jamii kuhusu usalama wa chanjo.
Bahati mbaya, sehemu ya watumiaji wa mitandao hawana weledi wa kutofautisha taarifa sahihi na potofu kuhusu chanjo.
Aidha, takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), zinaonesha kuwa zaidi ya wananchi milioni 16 wanapata taarifa kupitia mtandao wa intaneti.
Hata hivyo, watumiaji hawa hawana weledi wa kutosha kujua vyanzo sahihi vya taarifa kuhusu chanjo ya UVIKO-19. Aidha, uelewa mdogo wa matumizi ya mitandao umepelekea watumiaji wengi kuamini taarifa zinazopotosha ukweli kuhusu chanjo husika.
Hii ina maana kwamba, mitandao ya kijamii imekua kikwazo katika kujitokeza kwa wingi kwa wananchi ili kupata chanjo ya UVIKO-19 na hivyo kujikinga dhidi ya madhila ya ugonjwa huu hapa nchini.
Nini kifanyike?
👉Elimu na taarifa sahihi ya chanjo ya UVIKO-19 itolewe kwa waandishi wa habari wakiwemo Mabloga ili waweze kutoa taarifa kwa usahihi kuhusu chanjo kwa wananchi wengi.
👉Wizara ya Afya na wataalam wake watumie vyanzo mbalimbali vya habari ikiwemo mitandao ya kijamii, radio, televisheni, magazeti, na vipeperushi ili kutoa elimu sahihi na kuwahamasisha wananchi kuhusu chanjo ya UVIKO-19.
👉 Vyombo vya habari na mitandao ya kijamii nchini Tanzania vishirikiane na Serikali, hususan Wizara ya Afya, kutoa taarifa na elimu sahihi kuhusu umuhimu wa kuchanja na hatari ya kutochanja.
👉 Elimu na taarifa sahihi kuhusu chanjo itawaondolea hofu wananchi na hivo kujitokeza kwa wingi kupata chanjo.
Social Plugin