Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu Bi. Shemsa Mohammed (mwenye hijabu nyeusi) akiwa na viongozi wa CCM wilaya ya Busega akitembelea eneo la mgogoro vijiji vya Mwamkala na Mwagindi wilaya ya Busega
Na Costantine Mathias, Busega.
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Simiyu kimewataka wananchi wa vijiji vya Mwagindi na Mwamkala, kata Nyaluhande wilaya ya Busega kuwa wavumilivu wakati Chama na Serikali kikishughulikia mgogoro wa mpaka wa hifadhi baina yao na Wakala wa Misitu (TFS) katika eneo mashamba ambayo mipaka imepanuliwa na wakala huyo.
Hayo yamebainishwa jana na Mwenyekiti wa CCM mkoa humo Bi. shemsa Mohammed mara baada ya kutembelea mashamba ya wananchi ambayo yamemegwa na wakala huyo kwa ajili ya kutengwa kuwa hifadhi bila ya wananchi hao kushirikishwa mwaka 2012.
"Naombeni wananchi muwe wavumilivu, nikayafanyie kazi, nitakaa na Maliasili tushauriane ili mrudishiwe mashamba yenu...kwa nini waliweka mipaka ya awali na baadae kuihamisha?....katika hifadhi hiyo hakuna miti wala wanyama" amesema Shemsa.
Amewahakikishia wananchi hao kuwa mgogoro wa mipaka utamalizika muda si mrefu huku akiwaahidi kukutana na Waziri mwenye dhamana ili aweze kutatua mgogoro huo.
"Tutamfikishia Waziri, akishindwa nitamwomba Rais afike hapa, hatuwezi kupora ardhi ya wananchi bila kuwashirikisha, kuna makaburi na mashamba ya watu...tukae Chama na serikali ili mashamba ya watu yaweze kurejeshwa"amefafanua Mwenyekiti huyo.
Diwani wa kata ya Nyaluhande Maridadi Sabuni amesema jumla ya mita 830 ziliongezwa mwaka 2012 kutoka mpaka wa awali wa mwaka 1996 na kumegwa hekari 294 kijiji cha Mwagindi na hekari 360 kijiji cha Mwamkala.