Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SHIRIKA LA AGAPE LATAKA MTOTO WA KIKE ATHAMINIWE


Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Agape,John Myola.

Na Marco Maduhu, Shinyanga

Mkurugenzi wa Shirika la AGAPE mkoani Shinyanga John Myola linalotetea haki za watoto amesema wananchi wanapaswa kumthamini mtoto wa kike kwa sababu hana tofauti na wa kiume, zaidi ya maumbile ya kibailojia, na kuacha kuwabagua kwenye utekelezaji wa mahitaji yao hasa suala la elimu.

Akizungumzia siku ya mtoto wa kike Duniani ambayo hufanyika kila mwaka Oktoba 11, Myola amesema siku hii ni maalum kwa ajili ya kuikumbusha jamii kumthamini mtoto wa kike na kumpatia haki zake sawa na wakiume.


"Watoto wa kike wana akili sana darasani, mfano watoto ambao ni waathirika wa mimba na ndoa za utotoni tulionao hapa, ambao wanasoma kwa mfumo usio rasmi ufaulu wao ni daraja wa Pili na la Tatu, na wengine kwa sasa wapo vyuo vikuu, kidato cha Tano na Sita", alisema Myola.

"Watoto hawa walitaka kuzimwa ndoto zao, lakini sisi Shirika la Agape tukawachukua na kuwaendeleza, na sasa tuna waathirika wa mimba na ndoa za utotoni 63, na wanaendelea na masomo na wako vizuri kitaaluma," aliongeza.

Aidha, alisema wananchi mkoani Shinyanga, wanapaswa kubadilika na kuacha kutomthamini mtoto wa kike, bali wawapeleke shule ili kuja kuwasaidia hapo baadaye, kwa sababu mtoto wa kike huwa hasahau wazazi wake, na siyo kuzima ndoto zao kwa tamaa ya mifugo.

Katika hatua nyingine, alitaja vikwazo ambayo vimekuwa zikisababisha matukio ya mimba na ndoa za utotoni mkoani Shinyanga kuendelea kuwa ni pamoja na Sheria ya ndoa ya mwaka 1971, pamoja na baadhi ya watumishi wa vyombo vya dola kuzichukulia kesi za mimba na ndoa za utotoni kama vitega uchumi vyao.

Alifafanua kuwa, Sheria hiyo ya ndoa ya mwaka 1971 inaruhusu mtoto chini ya umri wa miaka 18, kuolewa kwa ridhaa ya wazazi au Mahakama, ambapo baadhi ya wanasheria huitumia kuwakinga watuhumiwa ambao ni wateja wao, na kuachiwa huru, jambo ambalo linasababisha matukio hayo kuendelea sababu ya wahusika kutofungwa jela.

Pia, alisema moja ya chombo cha dola (jina limehifadhiwa) baadhi ya watumishi wake siyo waaminifu kabisa, huku akitolea mfano wa kesi moja ya mtuhumiwa kumbaka mtoto, kuwa mmoja wao inasemekana alimwambia mtuhumiwa kuwa atafungwa jela miaka 30, bali atoe Sh.milioni Mbili ili kesi imalizike kimya kimya.

Myola alisema, ili mtoto wa kike aweze kulindwa na kupatiwa haki zake za msingi hasa elimu, ni lazima Sheria ya ndoa ifanyie marekebisho ya haraka, kwa kubainisha umri sahihi wa mtu kuolewa miaka 18, ili kutokinzana na Sheria nyingine zinazomlinda mtoto, pamoja na jamii kucha mila na desturi Kandamizi.

Aidha aliiomba Serikali, kuwasaidia msaada wa fedha kupitia mfuko wa benki ya Dunia, wa kusaidia watoto walioathirika na mimba na ndoa za utotoni, ili waweze kuwalipia ada ya shule watoto ambao wanawasomesha, sababu kwa sasa hawapo vizuri kiuchumi, kutokana na kutokuwa na mfadhili, ili watimize ndoto zao.

Nao baadhi ya watoto ambao ni waathirika wa mimba na ndoa za utotoni, walilishukuru Shirika la Agape kwa kutimiza ndoto zao zilitoka kuzimwa kwa kuwapatia elimu tena, huku wakiiomba Serikali kulishika mkono Shirika hilo, ili liendelee kuokoa ndoto za watoto wengi. 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com