Mwanariadha wa Kenya Agnes Tirop enzi za uhai wake
**
Mwanariadha wa Olimpiki wa Kenya Agnes Tirop ameuawa kwa kuchomwa kisu ndani ya nyumba yake eneo la Iten, Elgeyo, Kaunti ya Marakwet nchini Kenya leo Oktoba 13, 2021.
Mshindi huyo mara mbili wa medali ya shaba ya Mashindano ya Riadha ya Dunia, ambaye alimaliza wa nne katika fainali ya Olimpiki ya mbio za mita 5,000 miezi miwili iliyopita, alikuwa na umri wa miaka 25.
Uchunguzi wa jinai sasa unaendelea juu ya kifo chake, na polisi wanasema mumewe ametoweka.
Siku ya Jumatano, wachunguzi wa eneo la uhalifu walikuwa nyumbani kwa Tirop, ambaye polisi wanasema aliripotiwa kupotea na baba yake Jumanne usiku.
"Polisi] walipoingia nyumbani, walimkuta Tirop kwenye kitanda na kulikuwa na damu sakafuni," Tom Makori, mkuu wa polisi wa eneo hilo, alisema.
"Waliona alikuwa amechomwa kisu shingoni, jambo lililotupelekea kuamini ni jeraha la kisu, na tunaamini kwamba ndicho kilichosababisha kifo chake.
"Mumewe bado hajulikani aliko , na uchunguzi wa awali unatuambia kuwa mumewe ni mshukiwa kwa sababu hawezi kupatikana. Polisi wanajaribu kumtafuta mumewe ili aweze kuelezea kilichomsibu Tirop."
Makori ameongeza kuwa polisi wanaamini kuwa CCTV katika nyumba hiyo inaweza kusaidia uchunguzi wao.
Mshikilizi huyo wa rekodi ya ulimwengu mkenya Agnes Tirop pia alikutwa na jeraha la kuchomwa tumboni mwake.
Agnes Tirop wa Kenya alivunja rekodi ya ulimwengu ya mbio za kilomita 10 za wanawake huko Ujerumani mnamo Septemba
Rais Uhuru Kenyatta amejiunga na tasnia ya riadha nchini Kenya katika kumuomboleza Mwanariadha wa Olimpiki Agnes Jebet Tirop ambaye alikutwa amekufa nyumbani kwake katika mji wa Iten, Kaunti ya Elgeyo Marakwet Jumatano.
Agnes Tirop, mwenye umri wa miaka 25, alikuwa katika kikosi cha wanamichzo wa Kenya walioshinda mashindano ya Olimpiki ya Tokyo ya mwaka 2020 ambayo yalicheleweshwa ambapo aliiwakilisha nchi katika mbio za mita 5,000 na kumaliza katika nafasi ya 4 kwenye fainali.
Katika ujumbe kuifariki familia, marafiki, jamaa, na wadau katika mchezo wa riadha, Rais alimumboleza Agnes kama shujaa na bingwa wa Kenya ambaye kifo chake ni pigo kubwa kwa matamanio ya michezo na hadhi ya nchi.
"Inasikitisha, ni bahati mbaya kabisa na na jambo la huzuni kwamba tumepoteza mwanariadha mchanga na aliyeiletea nchi fahari akiwa na umri mdogo wa miaka 25, kupitia ushujaa wake katika riadha ya ulimwengu ikiwa ni pamoja na katika mashindano ya Olimpiki mwaka huu ya Tokyo ambapo alikuwa sehemu ya timu ya Kenya huko Japan, "Rais alisema
"Kinachosikitisha zaidi ni kwamba Agnes, shujaa wa Kenya, alipoteza maisha yake ya ujana kwa njia ya kitendo cha uhalifu kilichotekelezwa na watu wenye ubinafsi na waoga," Rais alisema, na kuamuru polisi kuharakisha msako dhidiya waliotekeleza mauaji yake .
"Ninasihi vyombo vyetu vya kutekeleza sheria vinavyoongozwa na Huduma ya Kitaifa ya Polisi wafuatilie na kuwakamata wahalifu waliohusika na mauaji ya Agnes ili waweze kukabiliwa na nguvu kamili ya sheria," alisema rais Uhuru .
Kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya nchini humo mwili wa Agnes, mshindi wa medali ya shaba ya Dunia katika mbio za 5000m na bingwa mwandamizi wa mbio za nyika mwaka wa 2015, ulipatikana katika nyumba yake huko Iten na majeraha ya kuchomwa na kisu .
Polisi kupitia ujumbe waliotuma katika twitter walihakikishia umma kwamba wataharakisha katika uchunguzi wa 'kina' kuhusu uhalifu huo .Ujumbe huo wa tume ya huduma kwa polisi pia ulituma risala za rambi rambi kwa familia ,marafiki na tasnia ya spoti nchini .
CHANZO - BBC SWAHILI
Social Plugin