MWANDISHI WA HABARI AIBIWA SIMU AKIITUMIA KURUSHIA MATANGAZO LIVE.... MWIZI AJIONESHA AKIVUTA SIGARA


Watumiaji wa mitandao ya kijamii nchini Misri wamempongeza mtu mmoja aliyejionesha uso wake kwa maelfu ya watu wakati alipokuwa akiiba simu ya mwandishi mmoja , 'kuwa mwizi mzuri zaidi Misri'.

Mahmoud Ragheb, ambaye ni mwanahabari wa kituo cha Youm7, alikuwa akiipeperusha hewani ripoti ya moja kwa moja kuhusu mitandao ya kijamii wakati mwizi huyo aliyekuwa akiendesha pikipiki alipokaribia na kuinyakua simu hiyo.

Bila kujua kwamba video ya simu hiyo ilikuwa hewani moja kwa moja aliitazama simu hiyo iliounesha uso wake wakati alipokuwa akitoroka eneo hilo huku akiwa anavuta sigara.

Kulingana na kituo cha habari cha Youm7, tukio hilo lilifanyika katika daraja moja lililopo katika mji wa nne kwa ukubwa nchini Misri ,Shubra Al Khaimah, ambapo bwana Ragheb alikuwa akirusha matangazo yake hewani kuhusu madhara yaliosababishwa na tetemeko la ardhi lenye kipimo cha 6.2 katika vipimo vya Richa, lililosababisha uharibifu mkubwa katika baadhi ya maeneo nchini Misri.

Bwana Ragheb alikuwa akichukua video katika daraja hilo wakati simu yake iliponyakuliwa katika mikono yake na mtu asiyejulikana. Wakati kamera ilipotulia iliuonesha uso wa kijana mdogo aliyekuwa akivuta sigara na wasiwasi mwingi iwapo kulikuwa na mtu ambaye alikuwa akimfuata.

Hatahivyo, hakuna aliyekuwa na huruma na mwanahabari huyo na badala yake watumiaji wengi wa mtandao walimuangazia mwizi huyo aliyekuwa akivuta sigara huku akitoroka.

Mtumiaji mmoja wa mtandao anasema alicheka sana , huku mwengine akihoji ni kwanini mtu huyo alikuwa akitazama nyuma kuona iwapo alikuwa anafuatwa ilihali ulimwengu wote ulikuwa ukimtazama yeye.

Zaidi ya watu 20,000 walikuwa wakitazama video hiyo ya moja kwa moja wakati wizi huo ulipofanyika.

Takriban watu 20,000 walikuwa wakitazama kanda hiyo ya video katika mtandao wa facebook. Kufikia sasa video hiyo imetazamwa na watu milioni 6.2 katika kipindi cha saa 24

Mwizi huyo alipatikana kwa urahisi alipokuwa akisakwa na mamlaka. Wizara ya masuala ya ndani ilitangaza usiku wa jana kwamba ilimkamata .

Katika taarifa , wizara ilisema kwamba mtu huyo hana kazi na kwamba amemuuzia mfanyabiashara mmoja simu hiyo.

Chanzo - BBC Swahili

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post