Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BUTIKU : WATANZANIA WATAENDELEA KUUENZI UONGOZI WA BABA WA TAIFA USIOLEA SUMU KWENYE UONGOZI

 Na Dotto Kwilasa - Dodoma

MKURUGENZI wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere Mhe. Joseph Butiku amesema miaka 22 bila uwepo wa muasisi wa Taifa hili Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, watanzania wataendelea kuuenzi  uongozi wake usiolea sumu kwenye uongozi na  kuondoa tofauti za kikabila zilizokuwa zikiitafuna nchi kwa wakati ule.

Butiku ameyasema hayo leo, Oktoba 14,Jijini Dodoma kwenye Kongamano la Vijana na Mwalimu Nyerere likiwa limewashirikisha baadhi ya watu waliowahi kufanya kazi na Baba wa taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere  ikiwa ni maadhimisho  ya siku ya kumbukumbu ya kifo chake kilichotokea  miaka 22 iliyopita nchini Uingereza katika Hospitali ya St.Thomas mwaka 1999.

Butiku ambaye aliwahi kuhudumu kama Katibu wa Mwl. Nyerere kwa miaka 21,amemtaja Nyerere kama shujaa wa ujamaa na kujitegemea hivyo kuwataka watanzania kujitegemea na kuacha uvivu utakaokwamisha maendeleo ya familia zao .

Aidha ameeleza kuwa maisha yake yalikuwa ni tunu kwa watanzania kwa kuwa aliishi kwa kusimamia uzalendo,umoja,mshikamano na kujitoa hata kwa kuhatarisha maisha yake.

Kutokana na hayo Butiku amesea vijana wa kitanzania wanapaswa kusimama katika nguzo hizo kwa kuzingatia malezi Bora ya wazazi wao na hatimaye kuwa na Taifa linalozingatia utu na maadili .

"Malezi yanawandaa watanzania wenye maadili na utii na kuwa na nafasi ya kukubali kusahihisha au kusahihishwa pale ambapo ni lazima,"amesema Butiku.

Pamoja na hayo ameeleza kuwa katika kipindi chote alichafanya kazi na Mwl.Nyerere alishukudia akiwajali  wanawake kwa vitendo na kuwapa usawa hali iliyowaondolea  dhana ya kudharauliwa .

Kwa kufanya hivyo amesema Nyerere aliamua kuandika kitabu cha wanawake ili kuhamasiaha jamii kutambua mchango wa wanawake katika harakati za maendeleo ya taifa.

"Tumeshuhudia Mwalimu akiwapa nafasi za uongozi baadhi ya wanawake akiwepo Titi Mohamed ",amesema

Kwa upande wake aliyewahi kuwa mbunge wa Bunge la Jamhuri ya muungano wa Tanzania kwa vipindi tofauti Steven Wasira ameweka wazi kufurahishwa na jinsi vijana wanavyomuenzi Mwalimu Nyerere kwa kujifunza mambo mengi aliyoyafanya katika kipindi uhai wake.

"Nimefurahi kuona kumbe kuna watu wanaomjua vizuri Mwalimu kama waliishi naye na hii inaonyesha wazi kwamba watanzania wanapenda Viongozi shupavu wanaojali uwajibikaji na uwazi Kama alivyofabya baba wa Taifa,"amesema

Mbali na hilo ameeleza kuwa Mwalimu Nyerere aliwajali vijana kwa vitendo kwa  kumpa kazi kwa nafasi ya ukuu wa Mkoa akiwa na miaka   27 tu.

"Vijana wasioelewa vizuri maono ya mwalimu wanaweza wakababaishwa sana kutokana na Dunia ya sasa ya mitandao,maisha mnayoishi sasa mnahitaji kukua zaidi kwa kuzingatia ukweli na hapo mtakuwa mmemuenzi ,"ameeleza.

Aidha amesema kutokana na mapenzi na nchi yake Mwalimu alianza harakati za utetezi akiwa bado mwanafunzi Ili kuondoa udini na ukabila ulioanzishwa na Wakoloni .

"Mwalimu alichukia ubaguzi wa kidini ulioanzishwa na wakoloni,wakoloni waliuchukia uislamu kitu ambacho Mwalimu aliopingana nacho na kuanzisha harakati za kupigania uhuru na hatimaye kuwa Taifa huru lisilo na udini,"amesema.

Mbunge anayewakilisha kundi la Taasisi zisizo za Serikali (NGO'S) Neema Lugangila ametumia nafasi hiyo kuikumbusha jamii kumuenzi Mwl.Nyerere kwa kuzingatia kilimo chenye tija kwa uhakika wa chakula na lishe.

Amesema,Baba wa taifa alikuwa muumini wa kilimo bora kwa kuamini kuwa ndicho kitakacho mkomboa mtanzania kuondokana na njaa pamoja na maradhi mbalimbali.

"Mwalimu Nyerere alipenda sana kilimo,aliamini kuwa kilimo ni uti wa mgongo wa Taifa letu,hii ilijidhihirisha wakati  akitoa mada maalumu huko Roma-Italia ambapo alisisitiza kuwa asilimia 97 ya watanzania kwa wakati ule wengi walitegemea sekta ya kilimo,"amesema. 

"Nakumbuka mwaka 1963 Nyerere alisema Tanzania kama taifa linapaswa  kufikiria kuimarisha tija ya kilimo chetu na kwamba ndo njia pekee ya kuinua kipato cha uchumi wa nchi jamba ambalo kwa vitendo kabisa  linaendelezwa na Rais wa sasa mama Samia kwa kuongeza fursa za ajira kwa vijana na lishe,"amesisitiza.

Amesema kupitia maadui watatu aliopingana nao Mwl.Nyerere, jamii inapaswa kuendeleza mapambano hayo kwa kuzingatia masuala ya lishe na kuondokana na viashiria vya utapiamlo.

"Tunategemea zaidi lishe  ili tuondokane na maradhi,hatuwezi kuwa na  maendeleo bila kuwa na afya njema,ni wakati wa vijana kushiriki katika sekta ya chakula na lishe,"amesema

Hata hivyo ameongeza kuwa ,uwepo wa chakula cha kutosha  haimaanishi uwepo wa afya bora kwani Mikoa inayolima vizuri mara nyingi inaongoza kwa kuwa na watoto wenye udumavu hivyo kuitaka jamii kuimarisha tija ya kilimo kwa uhakika wa chakula na lishe bora kwa nguvu kazi ya taifa.

Mbunge huyo pia hakusita kueleza fursa za vijana kupitia kada hiyo kuwa zipo nyingi kutokana na jitihada za Mwalimu Nyerere kuwaamini na kuwekeza kwa kuwapa nafasi za uongozi .

Amesema hali hiyo imewezesha sasa mashirika hayo kujitahidi kufanya kazi kwa uwazi na uwajibikaji ili kumuenzi Mwalimu Nyerere ikiwa ni pamoja na kuhusisha mipandgo na utekelezaji wake kwa uwazi.

Mbunge wa kundi la vijana Mkoa wa Singida Nusrat Hanje amesema katika kumuenzi Hayati Mwl. Nyerere lazima kuwaenzi pia Waandishi wa vitabu kwa sababu wamewezesha kizazi cha sasa kumjua vizuri.

"Wengi hatumjui Nyerere lakini kupitia Vitabu tunaweza kumuelezea sifa zake na kumuelewa,kupitia Waandishi wetu mahiri tuaishi kupitia maisha yake"amesema

Ameongeza kuwa ili kuyaishi malezi ya Mwl. Nyerere Serikali inapaswa kuwalea viongozi vijana ili kumuenzi kwa sababu aliwaenzi vijana kwa kuwatumia katika ujenzi wa Taifa,aliwaamini na kuwatengenezea mazingira mazuri ambayo sasa yanaonekana.

Hata hivyo ameeleza kuwa mbali na juhudi alizofanya Baba wa Taifa katika kuwekeza uadilifu kwa vijana,baadhi ya vijana hawana vielelezo vya kuaminika katika utumishi hivyo bado kunahitajika juhudi za kuboresha sekretarieti ya maadili ya viongozi wa Umma.

"Tusitangulize vyeo vyetu katika uongozi wetu,viongozi wengi ndiyo wanaohamasisha migogoro,waumini wa ubwana utakuta  hata milango ya magari yao wanafunguliwa wakati wana uwezo na nguvu za kufanya wao wenyewe,huu ni utumwa,tukitaka kweli kumuenzi Nyerere lazima tuache haya yote,"ameeleza Hanje.

Ameeleza kuwa kwa kukubali kuacha ubwana vijana wanaweza kuwa nguzo imara iliyoachwa  na baba wa taifa ikiwa ni pamoja na vijana wenyewe kukataa kunywanywaswa,kubaguliwa na kukubali kujisimamia wenyewe kwa kufuata kanuni na taratibu za nchi.

"Nyerere alisema tunahitaji kuona vijana jeuri wenye kuhoji mambo ya msingi  katika nchi hii,hatutaki vijana wa ndiyo bwana mzee,hapa alimaanisha Sisi vijana tukatae kuuishi utumwa ,hivyo sasa tuwe  chachu katika mapambano ya kupambana na ujinga,maradhi na umaskini ambavyo kama tungekuwa makini kwa kufuata haya mambo huenda pengine yasingekuwepo kwa ulimwengu wa Sasa,"amefafanua.

Licha ya hayo ameeleza kuwa ili kusimamia vyema rasilimali za taifa vijana wana wajibu wa kuishauri Serikali bila kuchoka kuhusu elimu inayotolewa na  kuwekeza fedha nyingi hali itakayosaidia kuondokana na maadui hao  watatu ambao Mwl.Nyerere aliwakataa.

"Wakati Dunia inatafakari namna ya  kuanzisha kwa magari ambayo hayana  dereva,sisi bado tunatafakari kuondoa ujinga na umaskini,lazima tujitafakari ,tunakwenda wapi,uelekeo wetu ni wapi,sera zetu za kisayansi ziko lazima tuziweke sawa kuyaishi maono ya Nyerere,"amesema.

Mbali na hayo ameeleza kuwa Tanzania kundi la vijana bado halina umoja unaotambulika hivyo kunatamani kuwe  na Baraza au chombo kimoja kinachowakutanisha vijana kama ilivyo  sehemu nyingi duniani.

"Tunahitaji tuone umuhimu wa sisi vijana kukutana kwa kukutanishwa na Baraza letu lenye lugha moja bila kutugawa,hiyo itakuwa namna Bora ya kumuenzi baba yetu wa Taifa ambaye katika kipindi chake chote hakuwahi kuwabagua vijana,"amesema.

Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya "Sisi Tanzania" ambao ndiyo waandaaji wa kongamano hilo Medoti Mashaka Medoti ameeleza lengo la kuandaa jukwaa hilo kuwa ni kuwapa fursa watanzania na hasa vijana  kumuenzi baba wa Taifa, kutafakari maisha yake na kuishirikisha jamii kuona ni kwa namna gani maisha yake yanakuwa chachi katika uchumi wa nchi.

"Tumelipa kongamano hili jina la Vijana na mwalimu Nyerere,tunatumia jukwaa hili kutoa mustakabali wetu kama vijana kwa kuziishi fikra zake hasa kwa kuzingatia katika harakati zake alitumia nusu ya maisha yake kuhudumia watanzania kwa kujitoa na kufanya misingi ya ujenzi wa Taifa letu kuwa na  dhana ya kuheshimu utu wa binadamu,"amesisitiza.

Pamoja na mambo mengine,Mkurugenzi huyo wa Sisi Tanzania, amesema kwa miaka  22 bila uwepo wa Hayati baba wa Taifa hili, watanzania wana kila sasababu za kujivunia kama taifa lenye mshikamano uliorithishwa.

"Katika hili tuna deni la kulipa kwa kushikamana kishirikiana katika kukemea ujinga na maradhi,tunamuenzi na kumkumbuka zaidi kwa uongozi wake usiolea sumu kwenye taifa letu na kuondoa tofauti za kikabila zilizokuwa zikiitafuna nchi kwa wakati huo,"amesema .

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com