Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

ANNE MAKINDA ATAKA ASASI ZA KIRAIA ZIHAMASISHE WANANCHI KUSHIRIKI SENSA YA WATU NA MAKAZI...KIWANGA ASEMA WAMEJIPANGA VYEMA


Kamisaa wa Sensa Spika wa Bunge mstaafu Anne Makinda akizungumza Akizungumza katika mkutano wa wadau wa Asasi za Kiraia kwenye Wiki ya AZAKI kuhamasisha wadau hao kuwafikia wananchi kuwapa elimu ya Sensa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Foundation for Civil Society (FCS) Francis Kiwanga akizungumza mara baada ya kumalizika alipokuwa akimkaribisha Mgeni rasmi Kamisaa wa Sensa Spika wa Bunge Mstaafu Mama Anne Makinda kwenye Mkutano huo uliofanyika leo Jijini Dodoma.
Kamisaa wa Sensa Spika wa Bunge mstaafu Anne Makinda akitoka akiwasalimia wadau na washiriki wa mkutano huo alipokuwa akitoka nje ya ukumbi baada ya kumalizika kwa mkutano huo.
Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-WAZALENDO Zitto Kabwe akipiga makofi akimpongeza Mama Anne Makinda mara baada ya kumaliza kuhutubia Mkutano huo.

Na: Hughes Dugilo, DAR ES SALAAM.

ASASI za kiraia nchini(AZAKI)zimetakiwa kushirikiana na Serikali kuhamasisha Wananchi kushiriki kikamilifu katika zoezi la Sensa ya watu na makazi itakayofanyika mwezi Agosti 2022. 

Akizungumza katika mkutano wa wadau wa Asasi za Kiraia kwenye Wiki ya AZAKI inayoendelea Jijini Dodoma, Kamisaa wa Sensa Spika wa Bunge mstaafu Anne Makinda ameeleza kuwa umuhimu wa sensa unagusa kila nyanja hivyo ni wajibu kwa kila mtanzania kuisadia Serikali kupata taarifa za msingi zitakazosaidia mchakato wa utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025, mageuzi ya masuala ya afya na jamii, pamoja na ufuatiliaji wa ajenda za maendeleo za kimataifa. 

"Sensa ni muhimu na inafanyika kila baada ya miaka kumi, ninyi watu wa AZAKI ni wadau namba moja ,tunatakiwa kutoka kwenye uchumi wa kati tuendelee zàidi tufanane na wenzetu,"ameeleza.

Amesema kuwa Sensa ya Watu na Makazi ni zoezi la kitaifa linalofanyika kila baada ya miaka 10 ambapo Sensa ya mwisho kufanyika nchini ni ile ya mwaka 2012 hivyo Sensa itakayofanyika itakuwa ni sensa ya sita kufanyika nchini tangu kupatikana kwa Uhuru na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964. 

Amesema kuwa kabla ya kupatikana kwa Uhuru zimewahi kufanyika Sensa nyingine tatu.

"Sensa ya watu na makazi ni utaratibu wa kukusanya, kuchambua, kutathmini, kuchapisha na kusambaza takwimu za kidemographia, kiuchumi na maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla, watu wote na makazi yao katika nchi kwa kipindi maalum, kwa maana nyingine, sensa ni zoezi maalum lenye lengo la kupata idadi ya watu wote katika nchi, kwa umri na jinsia, mahali wanapoishi na hali yao ya elimu, hali ya ajira, hali ya vizazi na vifo na hali ya makazi. Takwimu hizi za msingi ndiyo zinazoweza kuanisha mahitaji halisi ya wananchi yakiwemo makundi maalum yenye uhitaji maalum kwa mfano, watu wenye ulemavu, wanawake, watoto, vijana na wazee hivyo kurahisisha uandaaji wa sera na mipango ya maendeleo kulingana na uhitaji na mazingira yaliyopo,"amefafanua Makinda.

Kwa umuhimu huo, Mama Makinda ameeleza upekee wa Sensa hiyo kuwa utazingatia taarifa za idadi ya watu katika husaidia mamlaka za wilaya kutekeleza mipango ya maendeleo ambayo huakisi matakwa ya watu katika ngazi husika na kusaidia kwenye uwiano wa mgawanyo wa rasilimali. 

"Taarifa za sensa zitawezesha serikali kujua ongezeko la idadi ya watu, kwa mgawanyo na viashiria vingine, ambavyo ni muhimu kwa usimamizi wa mazingira, msingi wa utawala bora na ujumuishaji wa demokrasia, takwimu hizi zinahitajika kwa ajili ya ugawaji wa majimbo ya uchaguzi kwa ufanisi, kurekebisha mipaka ya kiutawala katika serikali za mitaa,"amesema.

Kwa upande wake Mtakwimu Mwandamizi, Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) David Mwaipopo ametumia fursa hiyo kuwaeleza wana AZAKI kuwa sensa ya mwaka 2022 kama zilivyo sensa zilizopita itatumia aina mbili kuu za Madodoso ambazo ni dodoso refu litakalotumika kuhoji asilimia 30 ya maeneo yote ya kuhesabia watu na Dodoso fupi litakalotumika kuhoji kwenye asilimia 70 ya maeneo yote ya kuhesabia watu.

Aidha ameyataja Madodoso mengine kuwa ni  la Taasisi ambalo ni mahsusi kwa ajili ya wasafiri, waliolala hotelini, nyumba za wageni, na waliolazwa hospitalini, na Dodoso la wasio na Makazi maalum ambalo ni mahsusi kwa watu wote wanaolala maeneo yasiyo rasmi, kwenye baraza za majengo mbalimbali, kwenye madaraja na maeneo mengine.

"Utekelezaji wa sensa ya watu na makazi hufanyika katika awamu kuu tatu kuu ambazo ni kipindi kabla ya kuhesabu watu, wakati wa kuhesabu watu na kipindi baada ya kuhesabu watu,"amesisitiza.

Licha ya hayo Mtakwimu huyo Mwandamizi amefafanua maswali yatakayoulizwa wakati wa sensa ya watu na Makazi huku akieleza kuwa moduli kumi na nne zitatumika kukusanya taarifa za watu na makazi yao kwa nchi nzima.

"Maswali hayo ni tarifa za kidemografia (umri, jinsi, uhusiano, hali ya ndoa, uraia, maswali yanayohusu ulemavu, tarifa za Elimu, maswali ya uhamaji, pamoja na taarifa za Watanzania wanaoishi nje ya nchi, mengine ni maswali kuhusu umiliki wa nyaraka za kitaifa, kama vile, vitambulisho vya NIDA, Mzanzibari mkazi, cheti cha kuzaliwa, hati ya kusafiria, na leseni ya udereva, pamoja na shughuli za kiuchumi na umiliki wa ardhi na taarifa za TEHAMA,"amesema.

Ameongeza kuwa maswali mengine yatakayoulizwa kipindi cha sensa  kuwa ni tarifa za uzazi na vifo vilivyotokea ndani ya kaya, vifo vitokanavyo na uzazia, hali ya nyumba za kuishi na umiliki wa rasilimali mbalimbali, maswali ya kilimo na mifugo pamoja na mifuko ya hifadhi ya jamii.

"Tunaomba AZAKI mshiriki kikamilifu kuelimisha jamii tufikie malengo,sisi kama Ofisi ya Takwimu tumejipanga vizuri kwa kutumia rasilimali chache zilizopo ili kukamilisha kwa wakati shughuli zote za maandalizi ikiwamo kazi ya utengaji wa maeneo ya kuhesabia watu katika ngazi ya kitongoji na mtaa ambayo ndiyo msingi wa kufanikisha sensa kwa ubora,"ameeleza.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Foundation for Civil Society (FCS) Francis Kiwanga, amesema kuwa wao kama Asasi za Kiraia wamejipanga vyema kuhakikisha wanashirikiana na Serikali katika kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi kutokana na mashirika ya Asasi za Kiraia kuwa karibu na wananchi kuanzia ngazi ya mashina, kata, vijiji na wilaya kupitia miradi mbalimbali wanayoisimamia kwenye maeneo hayo.

Tumefurahi kupata hiyo hamasa ambayo imetolewa vizuri sana na wataalamu na hasa sasa hivi Taifa letu linachangamoto ya kutoaminiana hasa kwenye mambo ya msingi kwahiyo sisi kama Asasi za Kiraia ni wajibu wetu kuhakikisha kwamba tunatoa elimu sahihi ya wananchi kueliwa umuhimu wa zoezi hili la sensa ya Kitaifa lakini pia elimu ya wananchi kushiriki zoezi hili muhimu la Sensa ya Kitaifa”

Aidha ameeleza namna ambavyo wao kama Asasi za kiraia watakavyoshiriki kuifikia jamii na kuihamasha kushiriki kikamilifu zoezi hilo na kusema kuwa Asasi nyingi zipo vijijini hivyo ni rahisi wao kuifikia jamii husika kwakuwa wao ni miongoni mwa wananchi wanaoshiriki nao kwenye miradi mbalimbali ya huduma za kijamii na maendeleo.

“Tunasema mbuzi kafia kwa muuza supu’ majukumu kama haya sisi ndio tuna uwezo mkubwa wa kuyasukuma na ndio nguvu yetu sisi kama Asasi ule ukaribu na wananchi na tunaamini kwenye hili taarifa sahihi zitafika kwa wananchi” Amesema Ameongeza Kiwanga. 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com