Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TANZANIA KUSHIRIKI MKUTANO WA KIMATAIFA WA MABADILIKO YA TABIA NCHI UINGEREZA

Waziri wa Nchi ,Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na mazingira Mh.Selemani Jaffo

 Na Dotto Kwilasa - Dodoma

TANZANIA inatarajia kushiriki Mkutano wa kimataifa wa mabadiliko ya tabianchi unaotarajiwa kufanyika tarehe 31,Oktoba hadi Novemba,12 Mwaka huu na kuungana na wajumbe wengine 3000 wa nchi mbalimbali Jijini Glasgow huko Uingereza.

Waziri wa Nchi ,Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na mazingira Mhe. Selemani Jaffo amesema hayo leo Oktoba 11,2021 wakati akitoa tamko la Serikali kuhusu ushiriki wake kwenye mkutano huo huku akieleza kuwa mkutano huo wa majadiliano utawahusisha viongozi wa Nchi na Serikali, Mawaziri na Wataalamu waliobobea katika masuala ya mabadiliko ya tabinchi.

Amesema,mkutano huo unafanyika katika kipindi ambacho Shirika la Umoja wa Mataifa la hali ya hewa Duniani limetoa taarifa inayothibisha  kuwepo kwa ongezeko la joto katika uso wa dunia na kuongezeka kwa kiwango cha joto kumesababisha athari za mabadiliko ya Tabianchi katika nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania.

"Athari hizo ni pamoja na kuongezeka kwa kina cha maji ya bahari kulikosababisha kisiwa cha Maziwe Wilaya ya Pangani na kisiwa cha Fungu la Nyani Wilaya ya Rufiji kumezwa na maji ya bahari", amesema. 

Ameeleza kuwa ushiriki wa Tanzania kwenye mkutano huo utaleta mafanikio zaidi na utasaidia kufungua uwekezaji wa sekta binafsi na miradi ya Asasi za Kiraia katika miradi ya mabadiliko ya tabia nchi.

"Ushiriki wa Tanzania katika Mkutano huu ni muhimu kwa vile utaiwezesha Tanzania kufaidika na fursa mbalimbali kama vile upatikanaji wa fedha na teknolojia zitakazosaidia katika juhudi za Serikali za kukabiliana na athari za mabadiliko ya Tabianchi,"amesema.

 Jaffo ameeleza kuwa Tanzania itashiriki kikamilifu katika majadiliano ya masuala yenye maslahi mapana kwa nchi na kuweka msimamo wake katika ya rasilimali fedha kwa ajili ya utekelezaji wa Mkataba na Makubaliano ya Paris.

"Kwa mujibu wa Mkataba huu, nchi zilizoendelea ziliahidi kutoa kiasi cha USD bilioni 100 kila mwaka ifikapo mwaka 2025 ili fedha hizi ziwezeshe nchi zinazoendelea kama Tanzania kuweka mipango na mikakati ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya Tabianchi,"amefafanua 

"Msimamo wa Tanzania katika suala hili ni kuzitaka nchi zilizoendelea kutimiza wajibu wao wa ahadi ya kutoa fedha hizi kama ilivyokubaliwa,kujenga uwezo wa Nchi zinazoendelea kama Tanzania ili ziweze kujiimarisha kwa ufanisi katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya Tabianchi na kuzijengea uwezo wa  kutekeleza majukumu yake kama yalivyoainishwa kwenye Mkataba na Makubaliano ya Paris,"ameeleza Jafo. 

Kuhusu Mkataba wa makubaliano ya kilimo na Mabadiliko ya Tabianchi,Waziri huyo mwenye dhamana ya mazingira nchini amesema kumekuwa na maoni kinzani kati ya nchi zilizoendelea na zinazoendelea kuhusu kujumuisha sekta ya kilimo katika sekta zinazotakiwa kupunguza uzalishaji wa gesijoto.

Amesema mchango wa uzalishaji wa gesi joto utokanao na shughuli za kilimo  ni mdogo katika nchi zinazoendelea ukilinganisha na nchi zilizoendelea.

Kutokana na hayo ameeleza kuwa Msimamo wa Tanzania ni kuwa, sekta ya kilimo isijumuishwe katika sekta zinazotakiwa kupunguza gesi joto kwa kuwa kilimo kinaathirika sana na athari za mabadiliko ya tabianchi kutokana na kutegemea mvua.

"Kuhusu uendelezaji na usambazaji wa teknolojia makubaliano ya Paris yanazitaka  nchi zilizoendelea kuziwezesha nchi zinazoendelea kutumia teknolojia mpya na za kisasa ambazo zitasaidia kuongeza uwezo wa nchi hizo kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi na kupunguza uzalishaji wa gesijoto, kwa kuwa Teknolojia hizo ni ghali na hazipatikani kirahisi,hivyo msimamo wetu katika suala hii ni kwamba nchi zilizoendelea zihakikishe nchi zinazoendelea zinapatiwa teknolojia hizo kwa gharama nafuu na kwa uwazi,"ameeleza.

Aidha ameeleza mchango wa Taifa wa kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi, Makubaliano ya Paris yanaitaka kila nchi mwanachama kuandaa Mchango wake katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambapo Tanzania iliwasilisha mchango wake kwenye sekretarieti ya Mkataba tarehe 30 Julai 2021. 

Waziri huyo ameyataja makubaliano mengine ya Paris yanatoa fursa ya nchi mbalimbali kushirikiana kwenye upunguzaji wa gesijoto kwa kutumia mbinu ya biashara na kueleza kuwa msimamo wa Tanzania ni kwamba nchi inayouza ziada ya upunguzaji isijumuishe kiwango kilichouzwa kwenye orodha yake ya upunguzaji ili kusitokee kuhesabiwa mara mbili kwani nchi iliyonunua ziada hiyo ndiyo itaweka kiwango hicho kwenye orodha yake ya upunguzaji gesijoto. 

"Pamoja na ukweli kwamba Tanzania siyo miongoni mwa nchi zinazozalisha gesi joto kwa wingi duniani, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imechukua hatua za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi zikiwemo kujenga uwezo wa kitaasisi, kutoa elimu kwa jamii na kuhimiza shughuli za kilimo, ufugaji na uvuvi zinazostahimili mabadiliko ya tabianchi,"amesema.  

Ameeleza kuwa katika kuungana na Jumuiya ya Kimataifa kupunguza uzalishaji wa gesijoto, Tanzania pia imechukua hatua stahiki zikiwemo Kuandaa Mpango wa Taifa wa Kupunguza Gesijoto (2021 - 2026),kuimarisha usimamizi wa misitu na program za upandaji miti,kuendelea na ujenzi wa Mradi wa umeme wa Bwawa la Mwl Nyerere; Ujenzi wa Reli ya kisasa na kuanza kutumika kwa gesi majumbani na kwenye uendeshaji wa mitambo viwandani .

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com