Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge akiongea wakati wa uzinduzi wa kampeni ya usafi wa mazingira.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Singida Zefrin Lubuva akizungumza
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Singida Yagi Kiaratu (katikati) akiongea na wananchi katika uzinduzi wa kampeni ya usafi wa mazingira .
Wananchi waliojitokeza siku ya uzinduzi wa kampeni ya usafi wa mazingira .
Na Edina Malekela, Singida.
Ni siku kumi na mbili tangu Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge kutoa agizo kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida kufanyika usafi kwenye fukwe za maziwa ya Singidani na Munangi wakati wa ziara yake ya kikazi aliyoifanya mwanzoni mwa mwezi huu,leo amezindua kampeni hiyo ya usafi wa mazingira.
Kupitia agizo hilo la Mkuu wa Mkoa sasa Halmashauri ya Manispaa ya Singida imezindua kampeni ya usafi wa mazingira ambapo kwa sasa usafi kwa Mkoa utafanyika kila Juma mosi.
Awali akisoma Taarifa Mkuu wa Idara ya mazingira Halmashauri ya Manispaa Arafa Mohamedi amesema lengo la kuzindua kampeni ya usafi wa mazingira ni kukumbushana na kuelimisha kuhusu wajibu wa kuhifadhi na kutunza mazingira kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Aidha Arafa amesema suala la uzururishaji ovyo wa mifugo katikati ya mji ni tatizo lingine linalosababisha uharibifu na uchafuzi wa mazingira ongezeko la watu na utiririshaji wa maji machafu katika mitaro na mifereji wakati wa mvua.
Alisema zipo jitihada zinazofanywa na Halmashaurj ya Manispaa ya Singida katika kukabiliana na changamoto za uchafuzi wa mazingira lakini kikubwa ni kuendeleza juhudi zilizoanzwa za kampeni ya usafi wa mazingira.
Naye Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Singida Yagi Kiaratu alisema kuwa wao kama Halmashauri watahuisha timu zote ili kuweka ulinzi wa Maziwa yasiendelee kuharibiwa na kuvamiwa na wananchi kwani maziwa hayo ni fahari ya Singida.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida Zefrin Lubuva alisema kuwa Halmashauri ya Manispaa ilipokea maagizo ya Mkuu wa Mkoa ya kusafisha fukwe za maziwa yote.
" Sisi Halmashauri ya Manispaa ya Singida pamoja na wananchi tulipokea maagizo yako na tunashukuru kwa kutuzindulia kampeni hii ya usafi wa mazingira na maono yako ya Singida safi inawezekana yatatimia",alisema Lubuva"
Aidha Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge wakati akizindua kampeni hiyo alimuagiza Mkurugenzi wa Halimashauri ya Manispaa ya Singida kusimamia sheria ndogo kwa wale watakao ingiza mifugo katika maziwa hayo.
"Mkurugenzi kuanzia leo ni marufuku watu kuingiza ng'ombe kuona ng'ombe kuzagaa kandokando ya maziwa yetu kwa sababu taratibu unazo wewe ni kuwatwanga faini tu hatutaki kuona mifugo kwenye maziwa yetu",alisema Mahenge"
Alisema kuwa maziwa hayo ni chanzo kizuri cha mapato kwa wale watakao kaidi agizo hilo ni kupigwa faini ya shilingi elfu hamsini huku elfu kumi ikibaki wa mgambo na elfu 40 kuingia kwenye mapato ya Halmashauri.
Aliongeza kuwa ni marufuku kwa wananchi kujenga vyoo ndani ya mita 60 kutoka kwenye ziwa ili kutunza mazingira na usafi wa maziwa pamoja na walaji wa samaki wanaopatikana katika maziwa hayo.
Social Plugin